Geita. Watu sita wamepandishwa kizimbani wakishitakiwa kwa kosa la mauaji ya aliyekuwa askari wa Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Julius Katambi, aliyeuawa Oktoba 20, 2023 akiwa lindo kwenye hifadhi ya Kigosi wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Washitakiwa katika kesi hiyo, namba 21464/2024, ni Mpandasabi Lutoja, Richard Mhozya (45), Mpejiwa Sumuni (35), Antony Sumuni (40), Majaliwa Marko (33) na Joseph William (28).
Washitakiwa wote wanakabiliwa na shitaka moja la kumuua kwa kukusudia Katambi kinyume na kifungu cha 196 na 197, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Akisoma maelezo ya awali ya shauri hilo, Wakili wa Serikali, Scolastika Teffe ameieleza Mahakama kuwa watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kosa la kumuua Katambi, aliyekuwa askari wa Tanapa, Oktoba 20, 2023 huko Mbogwe, Geita.
Amedai kuwa siku ya tukio, Katambi akiwa na wenzake kwenye doria katika Hifadhi ya Kigosi, waliwakamata watuhumiwa kwa kosa la kuchunga ng’ombe katika eneo la hifadhi na baada ya kukamatwa, walianza kumpiga marehemu sehemu mbalimbali za mwili wakitumia silaha za jadi, rungu na mapanga.
Amedai kuwa mabaki ya mwili wa marehemu yaligundulika Oktoba 31, 2023 na watuhumiwa wote walikamatwa kwa ajili ya mahojiano na mtuhumiwa wa tatu, wa nne na wa tano walikiri kutenda kosa la kumuua Katambi.
Kesi hiyo iliyokuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali, washitakiwa wote walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashitaka utakuwa na mashahidi 22 na vielelezo vinane.
Mawakili wanaowatetea washitakiwa ni George Alfred, anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Erick Lutehanga (wa pili), Jesca Godson (wa tatu), Yesse Lubanda (wa nne), Angel Kudra (wa tano) na Eliaman Ayoub (wa sita).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Geita, Kelvin Mhina anayesikiliza kesi hiyo, ameiahirisha hadi itakapopangwa tena na msajili kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.