Bashungwa awaondoa watendaji Kivuko cha Magogoni – Kigamboni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaondoa watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wanaosimamia usafiri wa kivuko kati ya Magogoni – Kigamboni na kuagiza kupangiwa kazi nyingine kwa kushindwa kusimamia kikamilifu huduma kwa wananchi wanaotumia kivuko hicho.

Walioondolewa ni Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Mhandisi Lukombe King’ombe na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni – Kigamboni, Idd Juma.

Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo leo Aprili 29, 2024 wakati akikagua huduma zinazotolewa na wakala huo na kusikiliza changamoto za wananchi wanaotumia usafiri wa vivuko kati ya Magogoni na Kigamboni na kuonyesha kutoridhishwa na utoaji wa huduma.

Katika ziara hiyo, Waziri Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kupeleka timu mpya ambayo itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za vivuko katika maeneo hayo.

Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa, akizungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri kuvuka katika kivuko cha Magogoni – Kigamboni baada ya kufanya ziara katika eneo hilo.

“Nikuagize katibu mkuu kuangalia namna ambavyo utawabadilishia mazingira na kuwapa
majukumu mengine Meneja wa Kanda na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni – Kigamboni na kuleta watendeji wapya ambao watamsaidia Mtendaji Mkuu kusimamia mkakati mpya wa maboresho ya TEMESA,” amesema Bashungwa.

Aidha amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, kuanza maboresho ya majengo ya abiria katika maeneo yote nchini yenye huduma za vivuko, ambapo ameelekeza kuanza kuondoa feni mbovu na kuweka mpya katika eneo la Magogoni – Kigamboni.

“Nimekagua na nimejionea mwenyewe sehemu ya jengo la abiria linahitaji maboresho na usafi, nimeona zile feni kwanza ikiwashwa unakimbia kwa vumbi lililopo. Unaweza ukapata madhara makubwa ya kiafya hivyo, zile feni ziondolewe mara moja na nimechukizwa na majibu yaliyokuwa yakitolewa sidhani kama Wizara kupitia TEMESA tunaweza kushindwa mambo madogo madogo kama haya,” amesema.

Kuhusu changamoto za mfumo wa malipo wa kukatia tiketi wa N – Card, Bashungwa amesema tayari timu zimeshafanya uchambuzi wa changamoto hiyo na Serikali inakwenda kuyafanyia kazi.

Pia ameiagiza TEMESA kuhakikisha wananchi wote wanaopata huduma za vivuko katika eneo la Magogoni na Kigamboni wawe wanalipa nauli kama mchango kusaidia uendeshaji wa huduma hiyo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema taasisi nyingi zilizopo kwenye mkoa huo zinafanya kazi kubwa na ameitaka pia TEMESA kuongeza ushirikiano kwa kuwa wao wanajihusisha moja kwa moja na wananchi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, amesema kwa sasa Kituo cha Magogoni – Kigamboni kina vivuko viwili ambavyo ni MV Kazi na MV Kigamboni vinavyotoa huduma kwa saa 24 na kufafanua kuwa kivuko cha MV Magogoni ambacho kimepelekwa kwenye matengenezo makubwa utekelezaji wake umefikia asilimia 55.2.

Related Posts