MIZANI 78 YAFUNGWA KUDHIBITI UZITO WA MAGARI

MKURUGENZI wa Idara ya Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Mhandisi Kashinde Musa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 27,2024 kuhusu ushiriki wao kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Meneja wa Mazingira na Jamii Wakala wa Barabara nchini Tanroad, Zafarani Madayi,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika kitaifa jijini Dodoma.


Na.Mwandishi Wetu-DODOMA.


SERIKALI imesema jumla ya mizani 78 imefungwa nchini kwa ajili ya kudhibiti uzito wa magari ili kuzilinda barabara ambazo hugharimu fedha nyingi katika ujenzi wake.


MKURUGENZI wa Idara ya Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Mhandisi, Kashinde Musa,ameyasema hayo leo Agosti 27,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika kitaifa jijini Dodoma.


Mhandisi Musa amesema kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara lakini moja kati ya changamoto zinazoharibu barabara ni suala la magari kubeba mizigo mizoto zaidi ya uwezo wa barabara.


“Niwatake wadau wote wa usafirishaji nchini kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za udhibiti wa mizigo barabarani ili barabara zetu ziweze kudumu kwa mujibu wa muda ule ambao umekusudiwa”amesema Mhandisi Musa.

Ameongeza kuwa ili kupunguza ongezeko la ajali nchini wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2024/ 2025 imetenga bajeti kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari katika majiji matano.

Ametaja majiji hayo kuwa ni Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es Saalam.


“Mradi huu utakapo kamilika tunatarajia utasaidia kupunguza ajali katika maeneo hayo lakini lengo letu ni kuhahakikisha maradi huu unakwenda nchi nzima”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa wizara imejikita katika matumizi ya teknolijia za kisasa kwa ajili ya kupunguza ajali katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufungaji wa Kamera za usalama.


“Kuna mradi wa majaribu wa ufungaji wa kamera ambao tuliufanya katika mikoa ya Pwani na Morogo mwaka 2016 ambao tumebaini kuwa tangu wakati huo tulipofunga Kamera hizo ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa sana hivyo lengo letu ni kufunga kamera hizo nchi nzima”amesema.


Kwa upande wake Meneja wa Mazingira na Jamii Wakala wa Barabara nchini Tanroad, Zafarani Madayi, amesema kuwa kila mtu anao wajibu wa kutunza miundombinu ya barabara.

Amesema kuwa , wananchi wanapaswa kutunza miundombinu ya baraba na kuacha kufanya shughuli zozote za kibinadamu kwenye hifadhi ya barabara.



Aidha, amewataka wanachi kuacha kuchoma moto na majani kwenye barabara pamoja na kupitisha mifugo ili kuepusha kingo za barabara kumegeka.

Related Posts