Huu hapa mtoko mpya wa Simba kimataifa

SIMBA ipo katika maandalizi kabambe kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Vijana hao wa Kocha Msauzi, Fadlu Davids, wanafahamu kwamba mpinzani aliye mbele yao wanayepaswa kumuondosha ili kufuzu makundi ni Al Ahli Tripoli ya Libya.

Al Ahli Tripoli inakwenda kucheza na Simba baada ya kuitoa Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya kucheza mechi mbili za hatua ya awali ambazo zote zimechezwa jijini Tripoli nchini Libya.

Simba walikuwa wakimsubiri mpinzani wa kucheza naye hatua ya kwanza baada ya kupata zali la kutoanzia hatua ya awali kutokana na kubebwa na renki yake katika mashindano ya CAF ikiwa ndani ya kumi bora.

Ili kuiendea vizuri michezo hiyo miwili ya ugenini na nyumbani, Kocha Fadlu ana nondo tano ameziweka tayari kuhakikisha hakuna kinachoharibika.

Ikumbukwe kwamba, mechi ya mkondo wa kwanza inatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 13 na 15 kwenye Uwanja wa Tripoli uliopo Libya, kisha marudiano ni kati ya Septemba 20 na 22 mwaka huu.

Katika mambo matano ambayo Fadlu anayo kwenye mpango kazi wake kuhakikisha Al Ahli Tripoli hawana sehemu ya kujiokoa na kipigo, ameuomba uongozi kumpa mechi mbili za kirafiki za kimataifa.

Uamuzi huo umekuja baada ya kikosi kucheza mechi ya mwisho ya kimashindano Agosti 25 mwaka huu ndani ya Ligi Kuu Bara kisha hakuna mechi nyingine hapo kati mpaka watakapovaana na Al Ahli Tripoli.

Kutoka Agosti 25 hadi Septemba 13 ambayo inatarajiwa kuchezwa mechi ya mkondo wa kwanza, Simba ina takribani siku 18, hivyo Fadlu ameona kukaa muda wote huo bila ya kucheza mechi itakayowapa kipimo sahihi itakuwa si sawa.

“Tunahitaji mechi za kirafiki zenye ushindani kabla ya kwenda Libya. Mwalimu anataka kuona maendeleo ya kikosi chake kabla ya kuwavaa Al Ahli Tripoli hivyo tunatarajia kuwa na mechi mbili za kirafiki zenye nguvu,” alisema kiongozi mmoja.

Taarifa ilizozipata Mwanaspoti ni kwamba katika mechi za kirafiki Simba inatarajiwa kucheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan inayonolewa na Kocha Frolent Ibenge. Al Hilal inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo hatua ya awali iliitoa Al Ahly Benghazi ya Libya na sasa inakutana na San Pédro ya Ivory Coast ili kutinga makundi.

Nondo nyingine inayoonekana kumpa jeuri Fadlu ni mbinu kuonekana kuanza kumlipa katika michezo aliyocheza.

Tangu kuanza kwa msimu huu 2024/25, Simba imecheza mechi nne za kimashindano zikiwamo mbili katika Ngao ya Jamii na zingine Ligi Kuu Bara.

Katika mechi hizo nne, Simba imeshinda tatu na kupoteza moja dhidi ya Yanga kwenye Ngao ya Jamii kwa bao 1-0.

Simba imeifunga Coastal Union katika Ngao ya Jamii bao 1-0, kisha Ligi Kuu Bara imetembeza vichapo dhidi ya Tabora United 3-0 na Fountain Gate 4-0.

Fadlu anayetumia mfumo wa 4-2-3-1 kwa maana ya mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji wawili na mshambuliaji mmoja, licha ya kujilinda sana, lakini timu yake ina uwezo wa kushambulia.

Katika mechi mbili za Ligi ambazo Simba imefunga mabao saba, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa, huku katika ulinzi ameendelea kuwaamini kipa Moussa Camara, mabeki Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Abdulrazack Hamza na Che Malone Fondoh, huku viungo wakabaji wakitumika Debora Fernandes na Mzamiru Yassin ambaye mechi dhidi ya Tabora alimpisha Augustine Okejepha kisha akampisha Yusuph Kagoma dhidi ya Fountain Gate.

Simba katika mechi nne ilizocheza za mashindano, Fadlu ameutumia mfumo wa 4-2-3-1 huku mwenyewe akisema anauona unakwenda kumpa matokeo kutokana na mambo mawili ambayo ni viungo wakabaji kufanya kazi kubwa  ya kusaidia ulinzi wakiwa na clean sheet tatu huku wakiruhusu bao moja na pia viungo wa ushambuliaji wakisaidia kupatikana mabao.

Wakati Al Ahli Tripoli wanacheza dhidi ya Uhamiaji, Simba walituma watu kwenda Libya kuwasoma wapinzani na waliporudi wakampa faili Fadlu na hivi sasa analifanyia kazi.

Mtoa taarifa kutoka ndani ya Simba, amebainisha kwamba katika kulifanyia kazi faili hilo, Fadlu amegundua wapinzani wao wanatumia mfumo wa 3-5-2 ambapo nyuma wanabaki mabeki watatu, na washambuliaji wawili. Pale kati viungo watatu wanaungana na mabeki wa pembeni wanaosaidia mashambulizi na kuzuia.

“Al Ahli Tripoli mfumo wao ni kutumia mabeki watatu wanaocheza zaidi nyuma, kisha wanajaza watu kwenye kiungo wakitumia mabeki wao wa pembeni kusaidia mashambulizi lakini kurudi kukaba.

“Ukiangalia mechi mbili walizocheza, aina ya mabao waliyofunga utagundua hilo, kuna kiungo wao mmoja alifunga mawili na straika akafunga mawili, hivyo kuna kitu Kocha Fadlu amekiona na anakifanyia kazi,” alisema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo aliongeza wamegundua wapinzani wao wanacheza soka la kasi, hivyo wanaamini hilo halitawapa shida kwa sababu nao wana wachezaji wa aina hiyo.

Katika mechi mbili dhidi ya Uhamiaji, wachezaji walioonekana kuibeba Al Ahli Tripoli ni mshambuliaji Ahmed Krawa’a mwenye miaka 35 aliyefunga mabao mawili sambamba na kiungo Ammar Taifour naye alifunga mawili.

Wakati huu ambao Simba haichezi mechi ya mashindano hadi itakapovaana na Walibya, kuna mechi za timu za Taifa ambapo nayo imetoa wachezaji kwenda kutumikia mataifa yao.

Hadi jana, wachezaji watatu walikuwa wamejumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachoingia kambini kujiandaa na mechi za kufuzu Afcon ambao ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Edwin Balua na Ally Salim, huku Valentino Mashaka akitarajiwa kujiunga na kikosi cha vijana cha Tanzania.

Kati ya wachezaji wanne wanaoanza kikosi cha kwanza ni wawili, Balua na Tshabalala ambaye ni nahodha, huku Mashaka akitokea benchi.

Mchezaji mwingine anayeanza kikosi cha kwanza anayetarajiwa kuondoka kwenda kulitumikia taifa lake ni kipa Moussa Camara, raia wa Guinea.

Kuondoka kwa wachezaji hao, Fadlu hataumiza sana kichwa kwani ataendelea kubaki na jeshi lake likiwa imara.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Al Ahli Tripoli, Fadlu alisema atazitumia vizuri siku zilizopo mbele yao kuhakikisha wanafuzu hatua ya makundi.

“Kuna kama wiki mbili za maandalizi kabla ya mchezo wa kwanza wa  CAF, tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ya aina gani, hivyo maandalizi yetu yataendana na hali hiyo.

“Kikubwa tunataka kufanya vizuri na kucheza hatua ya makundi, kisha baada ya hapo tutaanza hesabu zingine,” alisema kocha huyo.

Related Posts