Siku 40 Yanga, mboga moto, ugali moto!

JAMBO ambalo Yanga inapaswa kujivunia ni kwamba wachezaji wake nane tofauti wamefunga mabao 22 huku moja tu likiwa la kujifunga la timu pinzani, jambo linaloashiria kwamba timu hiyo haina tegemezi katika ufungaji msimu huu.

Lakini kinachofanywa na Yanga hapana shaka kinaumiza vichwa vya timu pinzani ndani na nje ya Tanzania katika kuangalia ni kwa namna gani zinaweza kuidhibiti kwa kile inachokifanya.

Kuanzia Julai 20 ilipocheza mechi ya kwanza baada ya kumaliza mapumziko hadi leo hii, Yanga imetimiza siku 40 ambazo imeonyesha ubabe wa nje na ndani ya uwanja.

Imetamba uwanjani kwa kuonyesha kiwango cha juu na kupata matokeo bora sambamba na mataji lakini nje ya uwanja imekuwa na neema ya kukusanya noti kiulaini.

Ndani ya siku 40, Yanga imecheza mechi nane za mashindano tofauti ambapo imeibuka na ushindi katika mechi saba na kupoteza moja tu ambayo ni dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani, Augsburg.

Katika mechi hizo saba ambazo imeshinda, moja ni ya Kombe la Mpumalanga dhidi ya TS Galaxy, nyingine Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs, pia katika kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi dhidi ya Red Arrows, zingine mbili ni za Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na Azam na mbili za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O.

Ni mechi ambazo zimeonyesha kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa Yanga kitimu hasa katika safu ya ushambuliaji na ile ya ulinzi na hilo linathibitishwa na takwimu zake katika mechi hizo.

Ukuta wake umeruhusu mabao manne tu katika mechi hizo nane ikiwa ni wastani wa bao 0.5 kwa mchezo na mawili kati ya hayo ilifungwa na Augsburg huku mengine ikiruhusu katika mechi dhidi ya Red Arrows na Azam.

Upande wa kushambulia, Yanga imekuwa moto mkali kwani katika mechi hizo nane, imefumania nyavu mara 23 ikiwa ni wastani wa mabao 2.9 kwa mchezo na hakuna mechi kati ya hizo ambayo ilimalizika bila Yanga kufunga bao.

Jambo ambalo Yanga inapaswa kujivunia ni kwamba wachezaji wake nane tofauti wamefunga mabao 22 huku moja tu likiwa la kujifunga la timu pinzani, jambo linaloashiria kwamba timu hiyo haina tegemezi katika ufungaji msimu huu.

Stephane Aziz Ki ndiye kinara akiwa na mabao sita akifuatiwa na Prince Dube mwenye mabao matano na anayeshika nafasi ya tatu ni Clement Mzize ambaye ana mabao manne.

Clatous Chama na Mudathir Yahya kila mmoja ana mabao mawili na Jean Baleke, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua kila mmoja amefumania nyavu mara moja.

Yanga katika kipindi hicho imefanikiwa kuchukua mataji mawili ambayo moja ni lile la Toyota ambalo ililipata baada ya kuifunga Kaizer Chiefs kwa mabao 4-0 na lingine ni Ngao ya Jamii ambalo ilibeba baada ya kuifunga Azam FC kwa mabao 4-1 katika fainali.

Wakati ikitamba uwanjani, Yanga imevuna kiasi cha fedha takribani Sh466 milioni ndani ya siku hizo 40 kutoka vyanzo tofauti ikiwa ni na wastani wa kupata Sh11.7 milioni kwa siku, Sh485,417 kwa saa na Sh8,090 kwa dakika na Sh134 kwa sekunde.

Kiasi kikubwa cha fedha imekipata kutokana na ubingwa wa mashindano ya Kombe la Toyota ambapo imevuna takribani Sh280 milioni, Dola 50,000 (Sh 136 milioni) imezinasa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika ambalo limetoa kiasi hicho cha fedha kwa kila timu inayoshiriki hatua za awali za mashindano ya klabu Afrika na Sh50 milioni imezipata kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Hassan ambaye anatoa kiasi cha Sh5 milioni kwa kila bao linalofungwa na timu ya Tanzania kwenye mashindano ya klabu Afrika hatua za mwanzoni.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema mafanikio wanayopata ni matunda ya uwekezaji ambao wameufanya na uongozi bora wa rais Hersi Said.

“Rais wa klabu, Mhandisi Hersi Said ni kiongozi mwenye maono na kwa kushirikiana na mdhamini wetu GSM na kamati yetu ya utendaji wamekuwa na malengo ya kuhakikisha Yanga inakuwa nembo ya mpira wa Afrika na kudhihirisha ukubwa wake kwa kutwaa mataji makubwa.

“Leo hii inajidhihirisha kwa namna Yanga inavyopata mafanikio makubwa ya nje na ndani ya uwanja ambayo yameonekana kuifanya izungumzwe Afrika nzima na kwingineko duniani. Sisi kama Yanga tunajivunia mafanikio haya na kwa mikakati ambayo uongozi wetu umeweka, tunaamini yatakuwa endelevu,” alisema Kamwe.

Related Posts