Wabunge walia gharama kwa wagonjwa wa figo

Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kutazama gharama za usafishaji wa damu kwa wenye magonjwa sugu ya figo nchini ‘dialysis’.

Wakati wabunge wakisema hayo Serikali  imewataka Watanzania kujinga kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi.

Changamoto hiyo inaelezwa wakati ambapo nchini kuna vituo vya afya 59 vikiwemo 29 vya umma vinavyotoa huduma za usaidizi wa kuchuja damu ‘dialysis’ kupitia mashine 649 za kusafisha damu, mpaka kufikia Januari 2024 mwaka huu.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya Januari mwaka huu, zinaonyesha Serikali hutumia kati ya Sh88.1 mpaka Sh110.2 bilioni kila mwaka kwa wagonjwa wasio na uwezo, wanaopata tiba ya kuchuja damu ‘hemodialysis’ kwa utaratibu wa misamaha.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo Jumanne Agosti 27, 2024, Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM) Zacharia Issaay amesema kwa kuwa Watanzania wengi wanakabiliwa na kadhia ya gharama za kusafisha figo, kwa nini Serikali haioni haja ya kutazama upya gharama ambazo kwa wiki ni Sh600, 000 hadi Sh800,000.

“Ukiangalia mwaka una majuma 56, gharama hii hailingani kabisa na maisha halisi ya Mtanzania. Serikali ina mkakati gani wa kupeleka huduma katika ngazi ya vituo vya afya vilivyojengwa, ili kupunguza gharama hizi na kununua vifaa pamoja na kuandaa wataalamu,”amesema.

Amesema hiyo itasaidia kupunguza gharama hizo kwa wananchi wanaopitia wakati mgumu wa matibabu kwa gharama hizo kuwa kubwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Serikali imeshafanyia kazi na kuwa katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam, gharama za kusafisha damu kwa wagonjwa hao ni Sh150,000.

Amesema gharama zinaendelea kushuka kwa jitihada zinazofanyika katika sekta hiyo ya afya na kwa sasa wapo katika ngazi ya mkoa.

Amefafanua kuwa hatua ya kwenda katika vituo vya afya, inahitaji uwekezaji mkubwa na utaalamu.

 “Suala si kujikita tunatibuje matatizo ya figo, bali tujikite kwa yale ambayo Profesa Janabi na wataalamu wengine wanayoyasema ili tusipate matatizo ya figo,”amesema Dk Mollel.

Katika swali la msingi, Issaay amehoji Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama za kusafisha figo kupitia bima ya afya kwa wote.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inafanya jitihada za kununua vitendanishi na vifaa vinavyotumika kusafisha figo moja kwa moja kutoka viwandani, ili kupunguza gharama za huduma hiyo.

“Nitoe rai kwa wananchi, mara utekelezaji wa bima ya afya kwa wote utakapoanza wajiunge  kwani ni njia pekee ya kuwasaidia kuepuka gharama za matibabu,”amesema.

Aidha katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amehoji kwa nini hatua ya kupunguza gharama hizo zilizofanyika katika Hospitali ya Temeke, zisifanyike kwenye hospitali nyingine nchini ili watu wengine waweze kuhudumiwa.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema lengo ni kwenda nchi nzima lakini wanaendelea kufanya hivyo kwa maana ya kubadilisha vifaa na vitenganishi.

“Lakini bado naendelea kusisitiza suala la magonjwa yasiyoambukiza tufuate maelekezo ya Profesa Janabi na wengine hapo ndipo tutaweza kutoka,”amesema.

Utafiti uliofanyika Kisarawe mwaka 2018 ulionyesha kati ya watu 100, 12 wana shida ya figo katika hatua tofauti tofauti.

“Kumekuwa na changamoto ya ongezeko la wagonjwa wanaofika na hatua za mwisho za kuchuja damu. Kwa wastani kwa wiki tunawapata wanne mpaka saba ambao wanahitaji kuchuja damu na wengi ni vijana, tunajaribu kutafakari sana kwamba changamoto hasa ni nini,” amesema Mkuu wa kitengo cha figo na Daktari bingwa mshauri wa magonjwa hayo BMH iliyopo Dodoma, Kessy Shija.

Hadi Januari 2024 takwimu za Wizara ya Afya zilionyesha jumla ya wagonjwa 3,500 wanapata huduma ya dialysis ikilinganisha na wagonjwa 1,017 ambao walikuwa kwenye huduma hiyo Agosti 2019 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Taarifa za Juni, 2023 zinaonyesha jumla ya wagonjwa 113 wamepandikizwa figo wakiwemo wagonjwa 78 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na 35 katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma.

Related Posts