Russia yalipiza kisasi kwa Ukraine

Wiki moja baada ya jeshi la Ukraine kuingia katika mipaka ya nchi ya Russia na kushambulia baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, kibao sasa kimegeuka.

Taarifa zinasema kuwa Russia nayo imejibu mashambulizi kwa kuvurumisha makombora nchini Ukraine, ikitumia ndege zisizo na rubani zilizolenga makazi ya watu na kusababisha vifo vya raia takriban wanne na kuharibu mitambo ya kuzalisha umeme.

Kwa mujibu wa mtandao wa Al Jazeera maofisa wa Ukraine wamethibitisha vifo hivyo vya raia wake wanne leo Agosti 27, 2024 na kuwa, watu wawili waliuawa katika shambulio hilo lililolenga hoteli iliyopo katikati ya mji wa Kryvyi na wengine wawili kuuawa kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye mji wa Zaporizhzhia nchini humo.

Kupitia ujumbe wa Telegram maofisa wa kijeshi wa Ukraine wamesema mifumo inayohusika na anga katika mkoa huo wa Kyiv ilitumwa mara kadhaa kwa usiku mmoja kurudisha makombora matano na ndege zisizo na rubani 60 zilizolenga utawala wa kijeshi wa mkoa huo.

Katika ujumbe huo wa Telegram, Serhiy Popko, Mkuu wa jeshi wa Kyiv, amesema vikosi vya anga vya Ukraine vimedungua drone takriban 15 na makombora  kadhaa karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, wakati wa shambulio hilo la Russia usiku.

“Kila kitu ambacho kiliruka juu ya mji mkuu wa Ukraine kiliharibiwa,” amesema kwenye Telegram.

Aidha, Ukraine imesema Russia ilirusha jumla ya makombora 91 na ndege zisizo na rubani 81 zinazodaiwa kuundwa na Iran katika mikoa kadhaa.

Jumatatu Agosti 26, 2024, Russia ilirusha zaidi ya makombora 200 na ndege zisizo na rubani na kuua watu takriban saba na kuharibu baadhi ya miundombinu ya nishati, huku Rais wa Marekani Joe Biden akilaani shambulizi hilo kwa Ukraine.

“Ninalaani kwa nguvu zote, kuendelea kwa vita vya Russia dhidi ya Ukraine na juhudi zake za kuwaingiza watu wa Ukraine gizani.”

“Wacha niseme wazi, Russia haitafanikiwa kamwe huko Ukraine na roho za watu wa Ukraine hazitakata tamaa kamwe,” amesema.

Hata hivyo, hakukuwa na maafa ya haraka yaliyoripotiwa kufuatia shambulio hilo la siku ya Jumanne.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameapa kupitia chapisho la X akisema, “Bila shaka tutaijibu Russia kwa shambulio hili na mengine yote.”

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mapigano hususan kwenye maeneo ya mipakani tangu uvamizi wa Russia Februari 24, 2022.

Related Posts