Dk Ndugulile wa Tanzania achaguliwa bosi mpya WHO Afrika

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile ameshinda nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Ukanda wa Afrika.

Katika kinyang’anyiro hicho wagombea wengine walikuwa pamoja na Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dk N’da Konan Michel Yao (Cote d’Ivoire) Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).

Dk Ndugulile amepata ushindi huo leo Jumanne Agosti 27, 2024 baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba (Niger) na nchi saba zikiipigia Rwanda.

Matokeo hayo yametolewa usiku wa leo Jumanne Agosti 27, 2024 katika Mkutano wa Afya wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea Brazzaville, Congo.

Mzunguko wa pili wa kuondoa mgombea mmoja, mgombea kutoka Niger alipigiwa kura 22 za kuondolewa, Rwanda kura 20 na Absteein alipigiwa kura 3.

Katika matokeo ya jumla ya mzunguko wa pili Dk Ndugulile alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita.

Dk Ndugulile ambaye ni mwanateknolojia, mtunga sera, mwanasiasa na mwakilishi wa wananchi, aliwakilisha nchi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania kinyang’anyiro hicho.

Kura hizo zimepigwa na Mawaziri wa Afya kutoka Kanda ya Afrika walioanza mkutano huo jana baada ya kufunguliwa na Rais wa Congo, Denis Sassou Ng’uesso.

Machi 11, 2023, Dk Faustine Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge duniani (IPU). Kwa uteuzi huo unaofanywa na Rais wa umoja huo wa mabunge duniani, ulimfanya Dk Ndugulile kuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu afya.

Uteuzi huo ulianza Februari mwaka 2023 ambao utadumu kwa miaka minne.

OKtoba 24, 2023 Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika jijini Luanda nchini Angola.

Kamati ya ushauri ya masuala ya afya, ina majukumu ya kushauri mabunge ya nchi na umoja wa mabunge duniani kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu afya.

Related Posts