Wasemavyo wadau uzalishaji umeme kwa njia mbadala

Dar es Salaam. Wakati lengo la Serikali likiwa kufikia uzalishaji wa megawati 1,100 za umeme kupitia njia mbadala mwaka 2025, wadau wametoa mapendekezo ya vitu vinavyoweza kufanywa na Serikali kukuza uzalishaji wa nishati hiyo kwa njia mbadala.

Miongoni mwa mapendekezo ni kupunguza gharama za ununuzi wa vifaa tofauti na ‘paneli’ za sola, kutowaona wadau kama washindani, kukuza uelewa kwa wananchi wajue umeme jua una nguvu kama umeme mwingine.

Wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti walipozungumza na Mwananchi hivi karibuni na wengine kutoa maoni wakiwasilisha mada katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu namna ya kuripoti habari zinazohusu nishati mbadala, hususani umeme jua kutoka Taasisi ya African Center for Media Excellence (ACME).

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Joyce Msangi amesema mpaka sasa Tanzania inazalisha megawati 2,171.75 za umeme kutoka vyanzo mbalimbli, lengo likiwa kufikia megawati 5,000 mwaka 2025 na megawati 10,000 mwaka 2030.

“Katika umeme tunaopanga kuzalisha hadi mwakani megawati 1,100 zinatakiwa kutokana na vyanzo mbadala, ikiwemo jua, upepo na joto ardhi,” amesema Joyce akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.

Amesema wanatambua kiwango kilichowekwa kama malengo ni ngumu kutekelezeka kutokana na muda uliobakia na kile kinachozalishwa hadi sasa, lakini kama Serikali ina utaratibu wa kufanya mapitio ya malengo yake na kuangalia kwa namna gani yametekelezeka na kupanga upya.

Amesema ili kusaidia suala hilo, Serikali iko mbioni kuzindua sera mpya ya nishati mbadala ambayo itasaidia utekelezaji wa baadhi ya majukumu.

“Lakini tunashirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyokuwa ya umma (NGO) na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya nishati mbadala,” amesema.

Haya yanasemwa wakati ambao tayari Tanzania imeanza ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa jua utakaozalisha megawati 150 ukiwa na thamani ya zaidi ya Sh323 bilioni unaotekelezwa katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Machi 14 2024.

Meneja Programu kutoka Taasisi ya Elico inayohusika na usambazaji huduma ya umeme wa jua, Adrian Mapunda amesema ili kufikia watu wengi zaidi ni vyema Serikali ikajikita katika usambazaji umeme na kuacha watu wengine wazalishe.

“Kama utapata mzalishaji zaidi ya mmoja ina maana bei ya umeme na ubora wake utaongezeka,” amesema.

Mapunda amesema uelewa wa wananchi ni jambo ambalo Serikali inaweza kusaidia hasa watu wakianza kufundishwa umuhimu wa nishati hiyo tangu wakiwa wadogo.

“Kitu kingine ni kupunguza gharama za kununua vifaa. Katika miradi mbalimbali ambayo Elico inafanya inashirikiana na mashirika mengine, wakiwemo wafadhili kupeleka vitu kama vile pampu, hivyo itusaidie kwa vingine kama kupunguza bei ya vifaa hivi,” amesema.

Vifaa vinavyozungumziwa ni pamoja na betri na taa akisema kwa paneli za sola tayari Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mapunda ametaka wadau wanaozalisha umeme wasionekane wapinzani, bali wanaosaidia kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo ambayo hayajafikiwa kwa kiasi kikubwa.

Ushirikiano na Serikali ni jambo lililozungumzwa, baadhi ya wazalishaji wa umeme wakieleza wanashindwa kufahamu mipango ya Serikali hasa ya upelekaji umeme katika maeneo wanayotaka kuwekeza, jambo linaloleta mkanganyiko baadaye.

Hilo linaelezwa ni kutokana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupeleka umeme miaka michache baada ya baadhi ya mashirika kuweka miradi yao, hususani inayohusu vituo vidogo vya kuzalisha umeme (mini gridi) na kusambaza katika makazi ya watu.

Fundi mkuu kutoka Kampuni ya Max Solar akizungumza na Mwananchi amesema kukosekana kwa uelewa ni sababu ya watu wengi kuendelea kuamini umeme unaozalishwa na vyanzo vingine tofauti na wa jua.

Amesema baadhi ya wakazi wamekuwa wakidhani umeme jua hauna nguvu ya kuwasha vitu mbalimbali, na hata nguvu ya kusukuma maji katika kilimo cha umwagiliaji.

“Tumekuwa tukitumia nguvu kuwaambia kuwa umeme jua unaweza kufanya chochote sawa na umeme mwingine, wakipewa elimu ya kutosha itakuwa rahisi kufikia watu wengi zaidi na kuuzalisha kwa wingi,” amesema.

“Kikubwa tunawaambia kutokana na jua kutopatikana muda wote ndiyo maana wanahitaji betri ili kutunza umeme uliozalishwa jua lilipowaka kwa saa nane hadi tisa,” ameeleza.

Ramadhani ameshauri kuwajengea uwezo mafundi walioko mtaani waweze kusaidia watu wengi na hata kutumika kwenye miradi mikubwa wanapohitajika.

Hayo yakielezwa, tafiti zinaonyesha upatikanaji wa umeme katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa miongo miwili iliyopita umeimarika hadi kufikia asilimia 49.9 ya idadi ya watu waliopo mwaka 2022.

Hata hivyo, wakati ufikaji umeme kwa watu ukiongezeka bado matumizi yake yako chini.

Kutokana na hilo, ipo nafasi kubwa ya umeme jua kutumika kama njia nyingine ya kuwafikia watu waishio vijijini, na ikitumika ipasavyo itachochea ukuaji wa kiuchumi wa watu.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa ACME, Kanda ya Afrika Mashariki kutoka nchini Uganda, Rachel Mugarura amesema umeme unaozalishwa na jua mbali na kutumiwa na watu wengi kama chanzo cha mwanga pia huweza kutumiwa kwa namna mbalimbali za kujipatia kipato.

“Umeme jua unaweza kutumika katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma jambo ambalo litachochea utengenezaji wa ajira,” amesema.

Rachel amesema matumizi sahihi ya umeme jua husaidia kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa chakula kutokana na kuchochea matumizi ya kilimo cha umwagiliaji hasa baada ya wakulima kuitumia kama njia ya kuzalisha umeme inayoweza kutumika kusukuma maji.

“Mbali na hilo pia hutumika kama njia ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza upatikanaji wa umeme,” amesema.

Related Posts