Ujenzi wa kudumu barabara, madaraja yaliyoharibiwa kusubiri mvua ziishe

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa amesema baada ya mvua kuisha wataanza kujenga barabara na madaraja ya kudumu katika maeneo yaliyoathiriwa.

Akizungumza leo Aprili 29,2024 baada ya kufanya ziara kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua katika Wilaya ya Kigamboni amesema kwa sasa wanarudisha mawasiliano ili barabara ziendelee kupitika wakati wakisubiri kupungua kwa mvua.

“Miundombinu imeharibika mikoa yote, mvua za vuli zimeunganika na masika lakini zimenyesha kwa kiasi ambacho hatujawahi kukipata katika kumbukumbu zetu.

Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa, akizungumza baada ya kufanya ziara kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua katika Wilaya ya Kigamboni.

“Hakuna barabara ambayo itakatika tushindwe kurejesha mawasiliano kutokana na namna mheshimiwa Rais anavyoiwezesha Tanroads katika kitengo cha dharura,” amesema Bashungwa.

Waziri huyo amesema pia Barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji ambayo awali ilipangwa kujengwa kilomita 41 sasa zimeongezwa kilomita 10 na zote zitajengwa kwa lami.

“Kigamboni ni wilaya muhimu kwa sababu Dar es Salaam ni jiji la kibiashara ambalo linatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu ikiwemo Kigamboni. Mvua zikikatika ujenzi wa barabara za kudumu utafanyika…sasa hivi tutarudisha mawasiliano,” amesema.

Bashungwa pia amemuagiza Mkurugenzi wa Matengenezo Tanroads, Dk. Christina Kayoza, kuongeza bajeti ili ujenzi katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua ufanyike haraka mawasiliano ya barabara yaendelee kuwepo.

Kuhusu eneo la Magogoni Kata ya Tungi ambalo pia lilikumbwa na mafuriko, Bashungwa amesema timu kutoka Tarura na Tanroads watafanya usanifu wa kina ili kutibu changamoto ya eneo hilo.

Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile, amesema kero kubwa ni mifereji ya barabara inayotoka Kongowe kwenda Mjimwema na kutoka Kibada kwenda Kisiwani.

Aidha amesema Barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji ni muhimu kwa wananchi wa Kigamboni ambapo kwa siku inapitisha magari zaidi ya 1,000 na kuiomba Serikali itengenezwe haraka kuwasaidia wananchi.

“Ujenzi wa barabara hizi na miradi ya DMDP utasaidia kuongeza wigo wa mawasiliano katika eneo la Kigamboni,” amesema Dk. Ndungulile.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema jiji hilo lina mifumo ya maji ya mvua lakini wapo wananchi waliojenga juu ya mifumo hiyo na kusababisha maji kukosa njia.

“Kuwe na timu maalumu itakayoonyesha ramani ili kuokoa kizazi cha Watanzania wengi, tukitaka kutibu tunahitaji kuumia kidogo ili mwakani tusiue watu,” amesema Chalamila.

Related Posts