Ili Tanzania tupate maendeleo ya kweli ambayo ni endelevu, ni lazima tujifunze kuukubali ukweli halisi jinsi ulivyo na kukitokea tatizo, tukabiliane nao kwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo na sio kufunika kombe mwanaharamu apite.
Ngorongoro kuna tatizo, Serikali ilitaka kulitatua kibabe, Wamasai wakagoma, alichofanya Rais Samia Suluhu Hassan ni kufunika kombe tu, lakini tatizo bado lipo na linahitaji ufumbuzi wa kudumu ili tuendelee kuwa na Ngorongoro yenye maendeleo endelevu.
Kufuatia hali ya Ngorongoro ilivyokuwa tete, jambo la kwanza ni pongezi kwa Rais Samia kunusuru Ngorongoro kwa kuepusha shari kwa mtindo wa funika kombe mwanaharamu apite, kwa kupooza tu, lakini ukweli unabaki palepale, Ngorongoro kuna tatizo, tutafute suluhisho la kudumu kwa kuwatendea haki wananchi wa Ngorongoro kwa mujibu wa Katiba, sheria, taratibu na kanuni.
Rais Samia ameupooza mtanziko wa Ngorongoro kupitia tamko la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi wakati akizungumza na wananchi wa kata 11 zilizopo tarafa ya Ngorongoro, akiwasilisha maagizo ya Rais aliyewatuma kuwasilikiza wananchi hao waliokuwa wamekusanyika na kukesha kwa siku tano wakitaka kujua hatima ya malalamiko yao.
Waziri Lukuvi alisema Rais ameagiza uchaguzi katika tarafa hiyo kwa kutumia mipaka ya zamani, ufanyike kama utakavyofanyika maeneo mengine nchini. Baada ya Rais Samia kuepusha shari Ngorongoro, Serikali iwawajibishe wale waliotufikisha hapo kwa kutotimiza majukumu yao kikamilifu.
Mwaka 1976, kulitokea mauaji ya vikongwe mikoa ya Mwanza na Shinyanga, Serikali kupitia Makamu wa Rais, enzi hizo, Rashidi Kawawa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Usalama, Peter Siyovelwa, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (DGIS), Emelio Mzena, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Samweli Pundugu na kamati za ulinzi za mikoa ya Mwanza na Shinyanga, walijiuzulu.
Katika mahojiano ya Mwanza, watuhumiwa wawili, Masaga Makhula Mazengenuka na Isaack Ng’wana Nkhobhoko wakapoteza maisha mikononi mwa polisi. Mwalimu Nyerere alisafisha wote kutokea juu kwa kuwastaafisha kwa manufaa ya umma, Kawawa akashushwa cheo, wakuu wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga wakafutwa kazi, maofisa wasimamizi, RPC, RSO, OCD na DSO, wote wakapandishwa kizimbani isipokuwa mshitakiwa mmoja tu, RSO wa Mwanza, aliyeponea tundu la sindano kutokana na kutetewa na wakili mahiri, Murtaza Lakha, lakini wengine wote walikula mvua za kutosha.
Hakuna tofauti ya kilichotokea Mwanza lakini mwaka 1976 na kinachofanyika Ngorongoro, kitendo cha Rais Samia kuingilia kati ni cha kupongezwa, lakini waliotufikisha hapo, wanapaswa kuwajibishwa na pili hatua za Rais Samia kuituliza hiyo hali ni funika kombe, tatizo la Ngorongoro bado lipo, litafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) lilianzishwa mwaka 1959 kwa Wamasai kutoka mbuga ya Serengeti kuhamishiwa Ngorongoro kama eneo la kipekee la matumizi ya mseto ambapo uhifadhi, utalii na maisha ya jadi ya jamii ya Wamasai vingeweza kuishi pamoja.
Idadi ya Wamasai ambayo ilikuja mwanzo kutoka Serengeti ilikuwa takriban 8,000 katika miaka ya 1959, sasa eneo hilo lina watu zaidi ya 100,000. Ongezeko hili la watu limeleta mzigo mkubwa kwenye rasilimali za eneo hilo, hali iliyosababisha uharibifu wa mazingira, ulishaji wa mifugo kupita kiasi na migogoro kati ya uhifadhi wa wanyamapori na shughuli za binadamu na wingi wa watu kutishia ekolojia ya eneo hilo. Japo mpango huu umelenga kuboresha hali ya maisha ya Wamasai ili wapate maisha bora na ya kisasa, unawahatarisha pia watu hao kupoteza uasili wao.
Malengo ya Serikali kuwahamisha Ngorongoro ni jambo jema lakini utekelezaji wake umekumbana na changamoto ikiwemo kuwalazimisha waliogoma kuhama, kutaka kuwahamisha kikuku kwa kutaka kutumia nguvu kwa kuvifuta vijiji na kuzuia vyakula huku akiwakatia huduma muhimu ili kuwashinikiza kuchagua kuhama au kufa njaa kwa Serikali kuvifuta vijiji vyao kinyume cha Katiba, sheria, taratibu na kanuni.
Alichokifanya Rais Samia ni kutuliza mtanziko wa tatizo kwa kulipooza, lakini tatizo bado lipo. Mapendekezo yangu ni; mosi, katika utekelezaji wa mpango huo, Katiba, sheria, taratibu na kanuni za uhamishaji zifuatwe.
Pili, ushirikishwaji wa wahusika kwa kuwatumia viongozi wa Wamasai wenyewe kwa kuanza na malaigwanani wao. Tatu, kufanya tathmini mpya ya kuwatambua Wamasai kama wakazi wa asili na kufanya upembuzi yakinifu nini kina faida zaidi kati ya binadamu na wanyamapori.
Binadamu wakiwa na faida zaidi kiutalii, wanyama ndio wapishe na Tanzania tuanzishe utalii wa wakazi asilia (indigenous people tourism) kama ilivyo kwa wahindi wekundu (red indians) huko Marekani, Aborigines huko Australia na Maori huko News Zealand.
Nne, jamii zote za asili za Tanzania, wakiwemo Wahadzabe, Wamang’ati, Watindiga, Wabarbaig, Wabalungi na jamii asili za makabila mbalimbali zitambuliwe zilindwe na zitunzwe kama kivutio cha utalii.
Tano, kitu muhimu kwenye taifa lolote, haiwezekani mnyama akathaminiwa kuliko binadamu, lakini huyu binadamu akizidi kuzaliana na kutishia ekolojia, lazima adhibitiwe, Marekani walitumia dawa ya kudhibiti uzazi ya Depo Provera, sisi tusifike huko.
Namalizia kwa kuuliza swali hili! Baada ya Rais Samia kuepusha shari kwa kupooza tuu kwa mtindo wa funika kombe, je, Watanzania tujifunze kuukubali ukweli wa tatizo, tutafute ufumbuzi wa kudumu wa tatizo husika, au tuendelee na huu mtindo wetu wa sasa wa kufunika kombe mwanaharamu apite?
Ukweli unabaki pale pale kuwa Ngorongoro kuna tatizo, je, tufunike kombe au tutafute suluhisho la kweli la kudumu kwa kuwatendea haki wana Ngorongoro kwa mujibu wa Katiba, sheria, taratibu na kanuni?