Zogo limesikika mitandaoni baada ya Rais, Samia Suluhu Hassan kutamka simba aliyewekwa bandani kwa ajili ya maonesho wakati wa Tamasha la Kizimkazi 2024, aitwe Tundu Lissu.
Kisha, akafafanua sababu ya kutaka simba yule aitwe Tundu Lissu. Pamoja na ufafanuzi, bado upo upande umeendelea kunung’unika. Hawajapenda. Je, unajua sababu ni nini? Kwa hali ya kawaida, kwa mtu yeyote angetafsiri alichomaanisha Rais Samia kumwita simba “Tundu Lissu”, kuwa ni utani wa kisiasa. Miguno ya kukataa simba kuitwa Lissu inabeba tafsiri kuna watu hawataki utani. Utamaduni wa Mtanzania, utani ni chachandu ya upendo. Wasiotaka utani, maana yake hawapendani. Iweje iwe hivyo wakati Rais Samia alishatambulisha falsafa ya R 4 ambazo ameahidi kuzitumia kulinda shughuli za kisiasa na kuimarisha demokrasia?
Lissu ni Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara. Rais Samia ni Mwenyekiti wa CCM. Ni viongozi wa vyama vyenye ushindani. Utani baina yao siyo tu ni kiashiria cha upendo kwao, bali pia ni msaada katika kupooza joto la kisiasa kwa wanachama na wafuasi wao.
Kwa nini utani unagomba? Jibu lake moja kwa moja ndiyo sababu inayohitajika kuelezwa kwenye aya ya pili. Rais Samia, alitaka maridhiano, ustahimilivu wenye kunyumbulika, mageuzi ya kisiasa na ujenzi mpya wa siasa za nchi. Hizo ndizo 4R za Rais Samia.
Binafsi, naamini 4R ni falsafa nzuri ya uongozi wa nchi. Swali, ni kwa nini baada ya miaka miwili ya Rais kutambulisha R 4, bado utani wa kisiasa unagomba? Mbona viongozi wa upinzani wanalia kupigwa na kuteswa na polisi?
Kujibu maswali hayo, ndiyo utaona tatizo la 4R lilipo. Ni hadithi yenye swali, kuku na yai kipi kilianza? R 4 za Rais Samia ni nzuri lakini ni kuku, kabla yake palipaswa kuwa na yai. Kwa nini 4R ziliibuliwa? Mazingira gani yalikuwepo kabla hadi yakasababisha umuhimu wa maridhiano, kustahimiliana, mageuzi na ujenzi mpya? Augusto Pinochet, aliongoza dola ya Chile kwa miaka 17 (1973 – 1990). Kipindi chake, watu wengi waliuawa, waliteswa na kupotezwa. Wanasiasa wa upinzani Chile, walijiona wapo jehanamu ndani ya taifa lao. Pinochet aliondolewa madarakani Machi 11, 1990. Akashika usukani Patricio Aylwin. Kitu cha kwanza ambacho alikifanya ni kuunda Tume ya Taifa ya Ukweli na Maridhiano. Mwenyekiti wa tume akawa Raul Rettig.
Tume ya Taifa ya Ukweli na Maridhiano chini ya Rettig, ilitoa ripoti yenye kuonyesha kila uchafu wa kisiasa enzi za Pinochet. Ripoti hiyo, maarufu kwa jina la Rettig Report, sababu ya Rau Rettig, ilitumika kujenga zama mpya za kisiasa Chile.
Rais Samia aliingia madarakani baada ya Dk John Magufuli ambaye zama zake maumivu ya wanasiasa yalikuwa dhahiri. Wapo waliofungwa jela na wengine hata kukimbia nchi. Kila lawama za wanasiasa wa upinzani zilipotoka, polisi walikuwa katikati.
Lakini kitu ambacho Rais alipaswa kufanya ni kuunda tume ya ukweli na maridhiano. Tume hiyo ingepitia madhila yote ya wapinzani wa kisiasa kwa ukweli kabisa, kisha maridhiano yangejengwa kutokana na kile ambacho tume ilikiona, lengo likiwa kuwezesha na kuchora mstari, yaliyotokea nyuma, yasijirudie.
Falsafa ya 4R ilipaswa kutambulishwa baada ya tume kufanya kazi yenye uchambuzi makini, kwa ukweli na yakini. Hapo maridhiano yangekuwa na nguzo. Shida iliyopo sasa ni kuwa maridhiano yalifanyika pasipo mzizi wa fitina kuchimbuliwa.
Mathalan, mzizi wa fitina baina ya polisi na wapinzani, dhahiri haukuchimbuliwa, ndiyo maana hali ni ileile, au imekuwa mbaya zaidi. Kipindi cha Magufuli, wapinzani walikamatwa, kuwekwa mahabusu na hata kufungwa. Wakati wa Samia, polisi wanapiga viongozi wa kisiasa hadi kuwaumiza. Maridhiano yamefanya kazi gani?
4R za Rais Samia zilileta mezani wanasiasa kujadili juujuu mkwamo wao. Laiti 4R zingetanguliwa na tume ya ukweli na maridhiano, mambo mengi zaidi yangeibuliwa. Pengine kusingekuwa na matokeo ya polisi kupiga viongozi wa kisiasa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika, aliyekuwa Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Salum Mwalimu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima Mdee na Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Kanda ya Serengeti, Esther Matiko, walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela au kulipa faini yenye jumla ya Sh350 milioni.
Katika kesi hiyo, walikuwepo pia mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa. Tume ilipaswa kuchunguza hili na kutoa majibu ambayo yangemwezesha Rais Samia kutunga 4R.
Ni zaidi ya miaka mitatu na nusu sasa Samia yupo madarakani, tamthiliya ya kuogofya ya watu kutekwa na kupotea inaendelea. Ingeundwa tume kuchunguza na kupata majibu ya wapi wtu hawa wako.
Jinsi hali ya kisiasa isivyo na utulivu, matukio yaleyale ya kipindi cha nyuma yanaendelea kutamalaki, kila kitu kinaleta jawabu kwamba lipo kosa la ufundi lilifanyika kabla ya 4R za Rais Samia. Tume ya ukweli na maridhiano ingepaswa kuanza kabla ya 4R.