Soko la Hisa Dar kuja na mikakati kuongeza ushiriki vijana, wanawake

Dar es Salaam. Ushiriki mdogo wa Watanzania hususan, wanawake na vijana katika uwekezaji kwenye soko la mitaji na dhamana umeusukuma uongozi wa soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), kuja na mikakati ili kulihamasisha kundi hilo.

Inaelezwa kihistoria makundi hayo hayapati fursa za mitaji na uwekezaji ndio maana ushiriki wao ni mdogo, hivyo kupitia elimu na ushirikishwaji kundi hilo limesisitizwa kutumia fursa ya kuwekeza katika soko la hisa ili kukua kiuchumi.

Ofisa Mtendaji Mkuu Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela amesema pia changamoto nyingine ni uelewa mdogo kutoka kwa umma wa Watanzania kuhusu uwekezaji katika soko la hisa.

Nalitolela ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 27, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital jijini Dar es Salaam. 

Amesema DSE imeweka utaratibu wa kupitisha kanuni zenye fursa maalumu kwa ajili ya kukusanya mitaji ya makundi hayo ikiwemo hatifungani zinazowalenga kinamama au vijana (Social, gender bond). Alitolea mfano hivi karibuni benki ya NMB ilikuja na hatifungani za wanawake na vijana na watu wenye uwakilishi hafifu katika masoko ya fedha.

“Katika mikakati ya kuongeza uelewa wa wananchi kwenye soko la hisa, suala lilipo ni kuweka mkondo rasmi kuanzia shuleni, sambamba na kutoa elimu kwa umma ili kuuchochea kushiriki,” amesema. 

Nalitolela amesema DSE kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na wadau wengine wamekuwa wakisisitiza uwepo wa utaratibu wa elimu ya ujuzi wa fedha na kuwekwa rasmi katika mkondo wa ufundishwaji shuleni.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya elimu utaratibu huu unafanyiwa kazi na utaanza kufundishwa mashuleni hivi karibuni ili watanzania wapate uelewa wa elimu ya uwekezaji kwenye fedha,” amebainisha.

Akifafanua zaidi amesema huwa wanashiriki tamasha la sabasaba kwenye wiki ya sekta ya fedha, kuongea na vyombo vya habari na kuchochea umma kupata shauku ya kuwekeza kwenye hatifungani na hisa ambazo zimeorodheshwa katika soko. 

Ametaja faida ya kuwekeza kwenye uwekezaji wa hisa ni uchumi kuongezeka pale kampuni inapopata faida na pale inapofanya vizuri na thamani ya hisa inaongezeka.

Aidha amesema kwa sasa Watanzania wameamka kwa kuanzisha makundi ya saccoss, vyama vya kuweka na kukopa kupitia ushiriki wa makundi hayo wanashirikiana nayo kutoa elimu.

“Soko letu linaendelea kukua na kufanya vizuri na jumla ya mtaji uliopo katika soko ni Sh17.4 trilioni. Pamoja na changamoto zinazotokea ulimwenguni kama Uvico19, vita vya Ukraine na Russia bado uchumi umeendelea kuwa imara,” amesema.

Amehakikisha soko kuendelea kukua kwa kuwawezesha wawekezaji wa ndani kwa kupata mitaji na kukuza biashara na kuwavutia wa nje kutokana na sera rafiki za kukuza biashara na uchumi wa nchi.

“Watanzania niwaambie soko la DSE liko kwa ajili yao na watapata faida kwa njia ya usalama mkubwa ukilinganisha na njia nyingine za uwekezaji,” amesisitiza.

Related Posts