Makonda azungumzia Uwanja wa Ndege Kisongo, amkaribisha Rais Samia Arusha

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda amesema Sh7 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kisongo mkoani humo unakwenda kubadilisha uchumi wa mkoa huo.

Makonda ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 28, 2024 alipokuwa akitoa salamu zake katika ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili ya Hazina (TR).

Amesema uwanja wa ndege wa Kisongo ni miongoni mwa viwanja vya mikoa vilivyo na miruko mingi ya ndege lakini kwa sasa unafanya kazi mwisho saa 11 jioni.

Hali hiyo imekuwa ikifanya wageni wanaokwenda Arusha kushukia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Sasa umetupatia Sh7 bilioni na sasa tunafunga taa, mkandarasi yuko kazini pia tuweze kuwa na njia ya kurukia ndege yenye urefu wa Kilomita 2.1 itakayotuwezesha ndege yoyote kutua usiku Arusha na kufanya shughuli za kiuchumi kuendelea kufanyika kwa ukubwa,” amesema Makonda.

Amesema uwekezaji huu utasaidia kuondoa foleni kutoka KIA kwenda Arusha ambayo imekuwa ikisababisha watalii kutumia muda mrefu katika foleni baadhi wakichelewa ndege na kufika wamechoka.

“Lakini kwa ndege za kutoka Arusha kwenda Zanzibar, uwanja wetu utakuwa na manufaa makubwa sana na nina imani jambo hili litakwenda kubadilisha kabisa uchumi wa mkoa wetu,” amesema Makonda.

Wakati hilo likifanyika Makonda amesema ipo haja ya kuwa na hospitali kubwa ya kimataifa katika mkoa wake ili kujenga utalii wa kimatibabu kutokana na kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.

“Natamani kuwa na hospitali kubwa ya kisasa iliyosheheni wataalamu wanaotoka mataifa mbalimbali ili kujenga imani kwa wale ambao hawajazaliwa nchini kutibiwa nchini,” amesema Makonda.

Makonda pia alitumia dakika hizo chache alizopewa kusalimia washiriki wa kikao kazi kumkaribisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maonyesho ya magari aina ya Landrover yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 12 hadi 14, 2024 mkoani Arusha.

Makonda amesema maonyesha hayo ni maandalizi ya kuvunja rekodi ya Guinness iliyowekwa na Ujerumeni kwa kuwa na magari aina ya Landrover 613 kwa wakati mmoja.

“Sisi mkoa wa Arusha tunaenda kuvunja rekodi kwa kuwa na magari 1000 kwa wakati mmoja, tutakuwa na maonyesho ya magari hayo na tunaalika wananchi wote nchini na nje ya mipaka kuja kuona vivutio lakini aina ya magari itakayotumika ni Landrover,” amesema Makonda.

Amesema ikiwa mtu ana Defender, Discovery, Jaguar atapokelewa kwa mikono miwili na tayari klabu mbalimbali zimeanza kusajiliwa.

“Tunakwenda sehemu ambayo tutakuwa na mchanganyiko wa Watanzania kutoka sehemu yoyote kuja Arusha kuchanganyika na wenzao. Kama kuna watu watatuonea wivu tunaomba radhi mapema ila tutakuwa na tukio la aina yake,” amesema Makonda.

Related Posts