KATIKA kile kinachoendelea kati ya mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kuhusishwa ama kutakiwa na klabu mbalimbali Afrika na Ulaya, viongozi wa timu hiyo ya wananchi hao wanapaswa kuwa makini juu ya jambo hilo.
Mzize kwa siku za hivi karibuni amekuwa akihitajika na klabu za Wydad AC ya Morocco na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambazo zimeweka mzigo wa kutosha kumng’oa kinda huyo.
Inaelezwa kuwa klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini iliweka Dola 200,000 ambayo ni sawa na (Sh542.3 milioni) ofa ambayo Yanga imetupilia mbali.
Mbali na Kaizer inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, aliyempandisha timu Mzize katika kikosi cha wakubwa wakati kocha huyo akiwa Jangwani pia Wydad ya Morocco inayofundishwa na Rhulani Mokwena wa Afrika Kusini nayo imeweka kitita cha Dola 100,000 (Sh271.1 milioni).
Lakini inaelezwa kuwa mabosi wa Yanga wameweka dau kubwa kwa klabu yeyote inayotamka Mzize kwa sasa ambapo italazimika kwenda mezani ikiwa na Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2 bilioni).
Yanga imemsainisha Mzize mkataba mpya kimyakimya unaomfanya aendelee kusalia ndani ya klabu hiyo kwa miaka miwili zaidi hadi mwaka 2027.
Mkataba wa sasa wa Yanga na Mzize ulikuwa unafikia tamati mwisho wa msimu huu, ambapo nafasi hiyo ukaziibua klabu nyingi ndani na nje ya nchi zikianza kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.
Hatua hiyo inaonyesha ni namna gani soka la Tanzania limekua kwa kiasi chake tofauti na awali kwani haikuwa rahisi mabingwa na klabu tishio kama Wydad kuja Tanzania na kutaka mchezaji tena mzawa.
Kumekuwa na mijadala mingi mitandaoni kila mmoja akizungumza lake lakini wengi wakitaka Mzize auzwe kwenda kutafuta maisha nje ya mipaka ya Tanzania.
Kubwa zaidi ni ofa zilizowekwa na timu hizo zimekuwa zikiwachanganya watu wakidai ni muda sasa wa Mzize kwenda kupiga pesa.
Lakini swali ni je, Yanga na wasimamizi wa mchezaji huyo hawataki pesa kama hizo? Au hawakuangalia hilo? Jibu ni hapana, hakuna mchezaji asiyetaka kucheza katika klabu kubwa kama Wydad.
Yanga inapaswa kuwa makini juu ya suala hili kutokana na mizigo inayoletwa mezani na kelele za mashabiki ambao kwa asilimia kubwa wanatamani kinda huyo atoke nje.
Ni kweli malengo ya Yanga msimu huu ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo na kufanya vizuri kimataifa lakini wanaweza kuwa bora kote huko bila hata ya kuwa na Mzize kutokana na nafasi na muda anaocheza.
Lakini kwa waliomfuatilia Mzize tangu anaanza kucheza Yanga utagundua kuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji tangu awepo Nabi ambaye alimsaidia kumpandisha na kumpa nafasi ya kucheza kikosi cha Jangwani.
Awali, Mzize alikuwa akipoteza nafasi nyingi anazopata na hata umaliziaji wake wa kuuweka mpira nyavuni haukuwa katika kiwango kizuri na kuwafanya mashabiki wamlalamikie hatua ambayo Gamondi amekuwa akipuuza na kumpa nafasi ya kucheza na msimu huu ameonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa.
Kwenye eneo la ushambuliaji kuna maingizo mapya, Prince Dube anayeonekana kuwa tayari kaingia kwenye mfumo wa Gamondi, Jean Baleke ambaye bado hajapata nafasi ya kuonekana na Kennedy Musonda ambaye alikuwepo msimu uliopita.
Ingawa sio mchezaji tegemeo lakini ukiangalia kwenye eneo hilo ukimuweka na Musonda kocha ataanza na Mzize ambaye ameonekana kuwa na muendelezo wa kiwango chake.
Yanga itapaswa kuwa makini zaidi hasa kwa eneo lake la ushambuliaji kwa kuwa kama itaamua kumuuza basi itahitaji ingizo jingine la mchezaji ambaye anafanana ama ataendana na Mzize.
Hata hivyo, kauli ya Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said kwenye moja ya mahojiano inaonyesha wazi kuwa bado wanahitaji huduma ya kinda huyo ingawa kwenye mpira wa miguu lolote linawezakana.
“Mzize ni tegemeo la taifa letu, makocha wote wawili wa Yanga (Nabi na Gamondi) wamempa nafasi, kwa sasa yuko kwenye mikono salama zaidi akiwa na jezi ya Yanga na ana mengi ya kujifunza na hapa ndio mahali sahihi kwake kwa maslahi ya timu yetu ya Taifa pia,” anasema Hersi.
Msimu wa 2022/23 ulipotamatika Yanga ilipambana kuhakikisha inambakiza mshambuliaji raia wa Congo, Fiston Mayele lakini ofa nono iliyowekwa na Pyramids ya Misri ikashika hatamu.
Karibu kila shabiki wa Yanga na baadhi ya viongozi hawakutaka ‘Mzee wa Kutetema’ aondoke klabuni hapo lakini kilichotokea pesa ikamuondoa na kumsafirisha hadi Misri.
Tangu alipoondoka timu hiyo ilikuwa ikikumbana na changamoto ya mshambuliaji ingawa Gamondi aliwatumia zaidi viungo wake Aziz KI, Pacome Zouzoua na Max Nzengeli lakini kuna muda lilionekana pengo lake.
Yanga pia inapaswa kujifunza hapa hadi leo bado hakuna mshambuliaji aliyeziba pengo lake ingawa kuna dalili za Prince Dube akauvunja ufalme eneo hilo.