Ukiteuliwa serikalini kutoka sekta binafsi hii inakuhusu

Dar es Salaam. Msajili wa Hazina wa Tanzania, Nehemia Mchechu amesema wako katika hatua za mwisho kuandaa programu maalumu kwa ajili ya watendaji wakuu wa taasisi hususan wale wanaotoka sekta binafsi wanapoingia serikalini ili waweze kuendana na mazingira yao ya kazi.

Mchechu ameyasema hayo leo Jumatano, Agosti 28, 2024 alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bidi na watendaji wakuu wa taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili ya Hazina (TR).

Kikao hicho cha siku tatu kinachofanyikia ukumbi wa mikutano wa kimataifa Arusha (AICC), kinafunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema program hii (induction program) ni jambo muhimu hasa kwa watendaji wakuu wapya wanaoteuliwa kutoka sekta binafsi ili wajue namna ya kufanya kazi ndani ya sekta za umma.

“Wakati mwingine watu wanakuwa hawajui namna ya kwenda tunajikuta tunawapoteza watu wazuri au tumewakatisha tamaa na morali waliyokuwa wamekuja nayo imepotea,” amesema Mchechu.

Amesema hilo linatokea bila kujua kuwa ipo namna au utamaduni ambao unapaswa kubadilishwa huku akibainisha zipo hatua watakazochukua kuhakikisha kuwa hilo linafanyika.

“Tutakusanya wateule wote katika ngazi ya watendaji wakuu walioteuliwa kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa hivi, nafikiri wamefika kama 94 nafikiri tuanzie hapo, hili ni zoezi litakalokuwa likifanyika sasa kila miezi sita, kundi lolote litakalokuwa limeteuliwa sasa ndani ya miezi sita watapitishwa kwenye programu hii,” amesema Mchechu.

Amesema programu hiyo itakuwa ikisaidia kuwapa maelekezo ya awali juu ya kazi za Ofisa Mtendaji na ikiwa ametoka sekta binafsi au serikalini basi waweze kuelewa changamoto zilizopo katika nafasi ya juu.

Katika hilo, Rais Samia amesema hilo ni jambo zuri huku akiwataka wale wanaowapokea wakurugenzi wanaoteuliwa kutoka sekta binafsi kuwapa ushirikiano.

Rais Samia amesema tuwape mafunzo na upande wa pili wale wanaopokea watu kutoka sekta binafsi tuwape mafunzo na msiwakwamishe.

“Tuwapokee na wanaowapokea tuwape ushirikiano ili mashirika yaende vizuri. Sio atake kufanya hili na mali lile muanze kusema aaaaaah, hatuendi hivyo,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa tuwape ushirikoano na wao wawape ushirikiano.

Mbali na hilo, Mchechu amesema ofisi yake inaendelea na uchambuzi wa kina katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache lakini haipati tija ya kutosha ambayo wanatarajia kuja na mapendekezo ndani ya miezi mitatu au miwili ijayo.

“Ripoti hii itatuonyesha kama lazima tuendelee kuwa na hisa huko au tuache wengine waendelee kuwa na hisa huko,” amesema Mchechu.

Wakati hili likifanyika, Mchechu amesema mageuzi mbalimbali yaliyofanyika katika taasisi za umma umesaidia kuongeza ushiriki wa taasisi katika uchangiaji katika mfuko wa serikali.

Hiyo ilifanya taasusu 211 sawa na asilmia 85 kuchangia katika mfuko huo ikiwa ni ongezeko kutoka taasisi 123 mwaka uliotangulia ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 49.

“Ukiangalia ukuaji huu muitikio ni mkubwa, changamoto tuliyonayo ni kwenda kuongeza mapato ya fedha ili tunapokuwa na idadi kubwa mapato yawe mengi zaidi,” amesema Mchechu.

Related Posts