Kesi ya ‘waliotumwa na afande’ kuendelea Agosti 30

Dodoma. Kesi ya jinai ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam inayowakabili washtakiwa wanne imeahirishwa hadi Agosti 30, 2024.

Hatua hiyo inalenga kupisha maamuzi madogo ya ombi la mapitio ya kesi hiyo lililofunguliwa Agosti 23, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 iliyoanza kusikilizwa Agosti 20 imetajwa leo Agosti 28 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

Ilisikilizwa kwa siku tano mfululizo kwa kusikiliza mashahidi watatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Agosti 23, 2024 Wakili Leonard Mashabara alifungua shauri la mapitio la kesi hiyo Mahakama Kuu.

Mashabara anaiomba Mahakama kufanya mapitio ya uhalali wa uwakilishi wa washtakiwa katika kesi namba 23476 ya mwaka 2024 inayowakabili askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Wakili Emmanuel Anthony anayemwakilisha Mashabara alisema wanaiomba Mahakama ijiridhishe na uhalali wa mawakili ambao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuwawakilisha au kuwatetea washtakiwa ilhali TLS kupitia Baraza la Uongozi lilitoa tamko Agosti 5, 2024 kwamba watuhumiwa ni wahalifu.

Anadai kupitia tamko hilo, TLS ilisema itashirikiana na vyombo vya haki jinai, hivyo wanaiomba Mahakama iseme kama ni halali kwa mawakili hao kuendelea kuwatetea washtakiwa hao.

Kutokana na kufunguliwa shauri hilo, hakimu aliahirisha kesi hiyo inayosikilizwa faragha hadi leo Agosti 28 kupisha maamuzi yatakayotolewa na Mahakama Kuu kuhusu maombi ya mapitio ya kesi hiyo.

Wajibu maombi katika shauri la mapitio ni Mahakama Kuu ni TLS, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mawakili wanaowawakilisha washtakiwa ambao wapo wanne na washtakiwa wenyewe.

Mahakama Kuu ilitoa muda wa siku tatu kwa wajibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani mahakamani hapo ambayo ilikuwa Jumatatu Agosti 26.

Hata hivyo, wajibu maombi walioko gerezani (Nyundo na wenzake) walishindwa kuwasilisha kiapo kinzani kwa wakati hivyo walipewa muda zaidi.

Nyundo na wenzake waliwasilisha kiapo chao jana Agosti 27, hivyo shauri hilo limepangiwa siku ya kusikilizwa.

Wajibu maombi hao (Nyundo na wenzake) leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili ya ubakaji wa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam lakini kesi imeahirishwa hadi Agosti 30.

Akizungumza nje ya mahakama leo Jumatano Agosti 28, 2024 wakili anayewawakilisha washtakiwa hao, Meshack Ngamando amesema kesi imeahirishwa kutokana na shauri la maombi ya mapitio lililofunguliwa Mahakama Kuu ambalo bado halijatolewa uamuzi.

“Kuna lile shauri la maombi ya mapitio ya kesi inayowakabili kina Nyundo na wenzake ambalo limefunguliwa Mahakama Kuu tuliambiwa tulijibu kwa kuleta kiapo kinzani sasa kesho (Agosti 29) ndiyo maamuzi madogo kuhusu shauri hilo yatatolewa na ndiyo maana kesi ya msingi imesogezwa mpaka Agosti 30 ambapo itaendelea kusikilizwa,” amesema Ngamando.

Related Posts