Mzava apiga ‘stop’ mbao za matangazo kubandikwa matangazo zabuni za serikali

Rungwe. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava ameagiza miradi yote ya serikali isitolewe zabuni kupitia mbao za matangazo.

Amesema badala yake itumike mifumo ya kidijitali ili kuweka uwazi na ushindani wa haki.

Hatua hiyo inalenga kuondoa malalamiko kuhusu zabuni kutolewa kwa watu wasio na sifa, udanganyifu, na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi kwa ubora unaostahili. Mnzava ametoa agizo hilo leo Jumatano Agosti 28, 2024, wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa kuboresha huduma za maji safi katika Mji wa Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, utakaohudumia vitongoji vinavyozunguka Kata ya Mabonde.

Mradi huo unatekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya-Uwsa), wenye thamani ya zaidi ya Sh3.67 bilioni na utahudumia wananchi 44,935. Hadi sasa, utekelezaji wake umefikia asilimia 90.

“Naagiza zabuni zote za manunuzi ya miradi ya serikali nchi nzima zitumie mifumo ya kidijitali na kuacha kutangazwa kwenye mbao za matangazo ili kuweka uwazi, uwajibikaji na kuondoa malalamiko ya watu wenye sifa kukosa tenda na wengine kupeana kiholela,” amesema Mnzava.

Aidha, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama na atawasiliana na waziri mwenye dhamana kuhakikisha fedha za kukamilisha ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1.5 zinafika kwa wakati.

“Napongeza Mamlaka ya Maji kufikisha huduma kwa wananchi kupitia tenki dogo. Nimesikia tayari Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Mwenyekiti wa Bodi wamefika na kuzungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhusu fedha za ukamilishaji wa tenki hili. Niwahakikishie mfumo wa malipo ukifunguka, mradi huu utakuwa wa kwanza kupokea fedha,” amesema kiongozi huyo.

Ameongeza kuwa; “Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu. Niwaondoe hofu, mfumo wa fedha ukifunguka mradi huu utakamilika mapema na kuongeza kasi ya utekelezaji na kujenga kwa ubora unaokidhi vigezo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mbeya-Uwasa, Gilbert Kayange amesema serikali iliagiza mamlaka za miji zifikishe huduma muhimu na kwamba, wamepewa dhamana ya kutekeleza huduma kwa jamii yenye changamoto.

Ameongeza kuwa mahitaji ya maji katika Mji wa Tukuyu ni lita milioni 15, lakini uzalishaji ni lita milioni tano.

Hivyo, amesema ujio wa mradi huo utazalisha lita milioni nane kutoka chanzo cha mto Mbaka na hivyo kuongeza uzalishaji hadi kufikia lita milioni 13 kwa siku.

“Tunashukuru kiongozi wa mbio za mwenge kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo, ambao utakamilika Desemba mwaka huu na wananchi kupata huduma ya maji safi kwa asilimia 95, kwa lengo la kutekeleza sera ya serikali ya kufikisha huduma kwa jamii na kumtua mama ndoo kichwani,” amesema.

Mbunge wa Rungwe, Athon Mwantona alimuomba Mnzava kuisukuma serikali kuleta fedha ili kukamilisha ujenzi wa tenki la maji katika mradi huo.

Mkurugenzi wa Uzalishaji Maji na Usambazaji, Barnabas Konga amesema mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa ‘force account’, kwa kuchimba na kulaza mabomba, na kazi inayoendelea ni kukamilisha ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita milioni 1.5.

Mkazi wa Kijiji cha Mabonde, Subira Athon ameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa mradi huo ili waweze kunufaika na kuondoa changamoto ya sasa.

Related Posts