NA WILLIUM PAUL.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi ameihoji Serikali imechukua hatua gani za muda mfupi wa kati na muda mrefu kunusuru theluji inayotoweka mlima Kilimanjaro.
Aidha Mbunge huyo katika maswali ya nyongeza, alihoji ikiwa Serikali ina mpango gani ya kuwatumia Wabunge wa mkoa wa Kilimanjaro katika zoezi la kuhifadhi mlima kwa kuwashirikisha kuhamasisha kupanda miti.
Pia alitaka kujua mipango ya Serikali kuwatumia watafiti wazawa kwa kuwashirikisha na kuwawezesha kufanya Tafiti badala ya kuwategemea wale wanaotoka nje ya nchi.
Akijibu swali hilo Bungeni, Naibu Waziri wa Mali asili na Utalii, Dunstan Kitandula amesema kuwa, sababu kubwa ya kupungua kwa barafu katika mlima Kilimanjaro ni kuongezeka kwa joto la Dunia kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu hususani ukataji wa miti, kilimo, uchomaji moto katika maeneo yanayozunguka mlima.
Alisema kuwa, katika kutekeleza mikakati ya muda mfupi serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kupanda miti takribani milioni 8 kwa mwaka katika mkoa wa Kilimanjaro sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.