Mwalimu mkuu ataja sababu vifo vya watoto sita bwawani, wanne wakizikwa

Rorya. Watoto wanne kati ya sita waliofariki dunia baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa la skimu ya umwagiliaji, Kijiji cha Ochuna wilayani Rorya, Mkoa wa Mara, wamezikwa kwenye eneo la pamoja katika kijiji hicho cha Ochuna.

Hata hivyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ochuna, Gasper Richard amefichua kwamba watoto hao walifariki dunia kutokana na kijiji kukosa maji safi na salama.

Baadhi ya majeneza ya watoto sita waliofariki dunia baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika katika bwawa la skimu ya kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Ochuna wilayani Rorya yakiingia kwenye uwanja wa shula ya Msingi Ochuna kwa ajili ya shughuli za mazishi.  Picha na Beldina Nyakeke

Wakati miili minne ikizikwa katika eneo la pamoja, miili mingine miwili ya watoto wa familia moja waliokuwa wakiishi na bibi yao kijijini hapo, ilichukuliwa na wazazi wao kwa ajili ya maziko nyumbani kwao, Kijiji cha Kamageta wilayani humo.

Watoto hao wote walikuwa wa kike na wanafunzi wa Shule ya Msingi Ochuna, walifariki dunia Agosti 24, 2024 jioni baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa la skimu ya umwagiliaji.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ochuna wakiwa kwenye uwanja wa shule yao kwaajili ya kuwaaga wenzao sita waliofariki dunia baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa la skimu ya kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Ochuna wilayani Rorya.  Picha na Beldina Nyakeke

Shughuli ya maziko imefanyika leo, Jumatano Agosti 28, 2024 katika eneo hilo la pamoja lililotolewa na mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake ni miongoni mwa waliofariki dunia.

Maziko hayo yameongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Rorya.

Miili ya watoto hao, iliyokuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Utegi, iliwasili katika uwanja wa Shule ya Msingi Ochuna saa 7:10 mchana.

Watoto hao sita wenye umri wa kati ya 9 hadi 12, walikuwa wanafunzi wa darasa la tatu hadi la sita ambao ni pamoja na Suzana Mwita na Unice Okumbe (darasa la tatu), Elizabeth Okumbe na Pendo Nyasanda (darasa la nne), Anjelina Suke (darasa la tano) na Evaline Sylvanus wa darasa la sita.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ochuna, Gasper Richard akizungumza wakati wa maziko amesema ingawa kifo hupangwa na Mungu lakini anaamini watoto hao walifariki dunia kutokana na kijiji kukosa maji safi na salama.

“Hawa watoto wamekufa muda si wao, hawakustahili kufa, ila wamekufa kutokana na kijiji chetu kukosa maji, laiti kama tungekuwa na maji safi na salama ya uhakika, watoto wasingefika huko bwawani na kumbukumbu zangu zinaonyesha hivi sasa watoto wanane wamefariki dunia kwa kuzama kwenye bwawa hili,” amesema mwalimu huyo.

Hivyo, ameiomba Serikali kukisaidia kijiji kupata maji safi na salama ili kuzuia matukio ya aina hiyo yasiendelee kutokea.

Pia, amesema shule imepoteza wanafunzi waliokuwa wakitegemewa kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ochuna, Erick Nyagandi ameiomba serikali kutekeleza mradi wa maji kijijini hapo na kutengeneza mazingira salama ya bwawa hilo.

Amesema hii ni mara ya pili kutokea kwa vifo katika bwawa hilo, mwaka 2004 watoto wawili walifariki dunia baada ya kuzama pia.

Mbunge wa Rorya, Jaffari Chege amesema eneo hilo linahitaji mradi mkubwa wa maji baada ya wa awali kushindwa kupata mafanikio.

Hivyo ameahidi kulichukua suala hilo na kulifikisha serikalini kusudi hatua za haraka zichukuliwe ili wananchi wapate uhakikisha wa maji safi na salama.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Chikoka amesema tukio hilo ni la kusikitisha na ni pigo kubwa kwa jamii ya Rorya na Taifa kwa ujumla.

Amesema baada ya kubaini changamoto ya ukosefu wa maji kijijini hapo, safari ya kutatua changamoto hiyo imeanza rasmi.

Shuhuda wa tukio hilo, Asteria Fataki akizungumza msibani hapo amesema alisikia kelele za watoto kuomba msaada kutokea majini, lakini akawazuia watoto wengine waliokuwa wanataka kuiingia majini kwa lengo la kwenda kuwaokoa wenzao.

“Baada ya hapo tukapiga kele za kuomba msaada zaidi kwa watu wengine, tusingewazuia wenzao huenda tungezungumza mengine, labda vifa vingekuwa vingi zaidi,” amesema shuhuda huyo.

Kufuatia tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi pamoja na msaada wa Sh30 milioni kwa familia zilizopata msiba huo.

Related Posts