AZAM FC jana ilikuwa uwanjani kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025 dhidi ya JKT Tanzania, lakini kabla ya mechi hiyo iliyopigwa jijini Dar es Salaam, mabosi wa timu hiyo wameshtushwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuzuia kwa muda mazungumzo ya mkataba mpya.
Fei Toto alisaini mkataba wa miaka mitatu ndani ya kikosi hicho, hivyo amebakiza mkataba wa takriban mwaka na miezi kadhaa, jambo ambalo liliwafanya matajiri wa klabu hiyo wajihami mapema kwa kutaka kumuongezea mkataba mpya, lakini walichokutana nacho kimewashitua baada ya kiungo huyo kuwagomea.
Ipo hivi. Mabosi hao walitaka Fei Toto apewe mkataba mrefu zaidi kutokana na kiwango alichokionyesha msimu uliopita na mechi za msimu huu, lakini mchezaji huyo amewataka wasiwe na haraka naye kwa sasa.
Azam ilitaka kumpa mkataba mnono Fei ambao ungemfanya kuwa kiungo ghali zaidi katika Ligi Kuu Bara, hasa baada ya kuifungia timu hiyo mabao 19 akimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya Stephane Aziz Ki.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimelidokeza Mwanaspoti kuwa, “Fei Toto bado kuna muda wa kufanya kazi naye, hivyo ameona hakuna haja ya kukimbilia hilo, kwani anaamini akifanya vizuri zaidi thamani yake itakuwa kubwa kuliko ofa aliyopewa kwa sasa.
“Pamoja na majibu yake ya kutotaka kujadili kwa sasa mkataba huo, hatujakata tamaa tunaangalia ni namna gani tunaweza kumshawishi ili kukubaliana na ofa yetu na ikibidi kuongeza zaidi, kwani huduma yake ni muhimu sana katika timu, hatutaki presha mbele ya safari,” alisema mmoja wa vigogo wa Azam.”
Wakati Fei akidaiwa kusitisha mazungumzo hayo, taarifa za uhakika zinasema kiungo huyo amekuwa na ofa nyingi kutoka klabu za ndani na nje ya nchi jambo ambalo ndilo linalowachanganya mabosi wa timu hiyo.
Inadaiwa klabu za Wydad Athletic ya Morocco inayofundishwa na kocha Rhulani Mokwena na Kaizer Chiefs ya kocha Nasreddine Nabi aliyewahi kufanya kazi na Fei wakiwa Yanga pamoja na Simba zimekuwa zikitajwa kumfukuzia kiungo huyo wa zamani wa JKU ya Zanzibar na Singida United.
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa ya Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alipotafutwa kufafanua juu ya madai hayo alidai hawezi kusema lolote, kwani alikuwa bize na mechi ya jana dhidi ya JKT Tanzania iliyokuja baada ya siku chache tangu timu hiyo itolewe raundi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.