Kilichompa ushindi Dk Ndugulile WHO hiki hapa, azungumza

Dar es Salaam. Maswali ya papo kwa papo yaliyojibiwa kwa ufasaha, ni miongoni mwa mambo yaliyompa ushindi mteule wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile.

Dk Faustine Ndugulile anachukua nafasi ya Dk Matshidiso Moeti aliyehudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Nchi wanachama wa Afrika zilipiga kura kumteua Dk Ndugulile wakati wa kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO, kilichofanyika Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, jana Jumanne Agosti 27, 2024

Kikao hicho ambacho hufanyika mara moja kwa mwaka, hujadili na kuidhinisha sera, shughuli na mipango ya kifedha inayolenga kuboresha afya za watu wa Afrika.

Uteuzi wa Dk Ndugulile utawasilishwa katika kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji ya WHO kitakachofanyika Februari 2025 huko Geneva, Uswisi kwa ajili ya kuidhinishwa.

Mkurugenzi wa Kanda aliyeteuliwa (Dk Ndugulile) ataanza kazi baada ya jina lake kuidhinishwa na bodi hiyo na atadumu kwa miaka mitano. Baada ya muda huo cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO, ataketi tena kutathmini utendaji wake iwapo atastahili kuendelea kwa kipindi kingine cha pili.

Akinadi sera zake kabla ya upigaji kura, Dk Ndugulile alitaja huduma bora za afya, mawasiliano na uboreshaji wa mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa kitakua kipaumbele chake.

Alisema endapo atachaguliwa, atahakikisha Waafrika wanapata haki ya kupata huduma bora za afya, kuboresha utayari wa nchi za Afrika katika kukabiliana na majanga ya magonjwa ya mlipuko, kuimarisha uwajibikaji ndani ya WHO kanda ya Afrika pamoja na kuimarisha mawasiliano baina ya nchi wanachama katika masuala ya afya.

Baada ya kunadi sera zake, Dk Ndugulile alipokea maswali manne ya papo kwa papo kutoka kwa mawaziri wa afya waliowakilisha nchi zao na kufanikiwa kuyajibu kwa ufasaha.

Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na namna atakavyokabiliana na changamoto ya muingiliano wa magonjwa hasa ya mlipuko na mabadiliko ya tabia nchi.

Akijibu swali hilo, Dk Ndugulile alisema mabadiliko hayo yamekuwa yakiathiri nchi nyingi, hivyo ikichaguliwa atashirikiana na wajumbe wengine kuandaa mpango na kushirikisha wadau wa kijamii na kiuchumi pamoja na kuwekeza katika tafiti, ili kupata takwimu sahihi na kupata suluhisho la changamoto hiyo.

Swali lingine lilihoji namna atakavyopata fedha za kushughulikia masuala mbalimbali ya kiafya Afrika, akijibu alisema pia atatoa hamasa kwa nchi mbalimbali kuhakikisha malengo ambayo nchi wanachama wameyaweka, yatekelezwe ili kufikia malengo.

“Mawasiliano baina yetu ni muhimu, hatutakiwi kushindana, tunatakiwa kufanya kazi pamoja kuwa na ajenda moja kikanda. Kuna makosa mengi tunayafanya kama ukanda, tunapaswa kukaa meza moja ili kutimiza viashiria vya utendaji kazi, kwani kila nchi imejiwekea malengo yake,” alisema Ndugulile.

Licha ya kampeni zilizofanywa, Dk Ndugulile alikuwa na nafasi kubwa ya ushindi kutokana na nafasi mbalimbali alizowahi kushika ndani na nje ya nchi.

Machi 11, 2023, Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na kuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.

Oktoba 24, 2023, achaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo katika uchaguzi uliofanyika Jijini Luanda, nchini Angola.

Katika salamu zake baada ya kuteuliwa jana, Dk Ndugulile alieleza dhamira ya kuendeleza afya za wananchi wa ukanda huo.

“Nimeheshimiwa sana na nimenyenyekea kuchaguliwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya WHO barani Afrika. Nashukuru nchi wanachama kwa imani iliyoonyeshwa kwangu. Naahidi kushirikiana nanyi, na ninaamini kwa pamoja tunaweza kujenga Afrika yenye afya njema,” amesema Dk Ndugulile.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, leo Jumatano Agosti 28, 2024 ameandika akishukuru kwa heshima aliyopewa kuchaguliwa katika nafasi hiyo.

“Ninawashukuru mawaziri wa afya kutoka nchi wanachama kwa imani yao katika uwezo wangu. Natanguliza shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa msaada wake usioyumba wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na kwa ujumbe wake wa pongezi.

“Napenda pia kuwapongeza washiriki wenzangu kwa kampeni zao kali. Nimesoma mawasilisho na ilani zenu na ninatambua mchango wa kipekee ambao kila mmoja wenu anaweza kutoa, ili kuimarisha afya ya bara letu na nitakuwa nikiwafikia,” ameandika.

Dk Ndugulile pia alitumia nafasi hiyo kutuma ujumbe kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, akimshukuru kwa kazi nzuri anayoifanya.

“Nitafanya kazi nanyi kwa karibu ili kuendeleza ajenda ya afya katika bara zima la Afrika. Natoa shukrani zangu kwa Dk Moeti kwa uongozi wake bora katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na ninajitolea kuendeleza ajenda ya mageuzi ambayo alianzisha,” ameandika.

Pia amesema anatarajia kushirikiana na washirika na washikadau katika siku zijazo ili kuweka mikakati ya jinsi ya kufikia mustakabali mzuri wa Afrika kwa pamoja.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wanaume na wanawake wote waliounga mkono kampeni hii kwa nyadhifa mbalimbali, michango yako imekuwa ya thamani sana,” ameandika.

Wagombea wengine walioshiriki uchaguzi huo ni pamoja na Dk Boureima Sambo (aliyependekezwa na Niger), Dk Ibrahima Fall (aliyependekezwa na Senegal) na Dk Richard Mihigo (aliyependekezwa na Rwanda).

Watu mbalimbali wametuma salamu za pongezi, akiwemo Rais Samia aliyesema ana imani kubwa na Dk Ndugulile.

“Pongezi za dhati kwa Dk Faustine Engelbert Ndugulile kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika. Umeifanya nchi yetu kujivunia na bara letu litafaidika sana na kazi yako.

“Nina imani kwamba ujuzi na uzoefu wako katika sekta ya afya utaiwezesha Afrika kuwa na sauti muhimu katika ngazi ya kimataifa, katika kukabiliana na changamoto za afya kwa mamilioni ya watu wetu katika bara zima. “Nakutakia kila la kheri na mafanikio mema,” amesema Samia.

Pia Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza katika mkutano wa wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za Serikali leo Jumatano jijini Dodoma, amempongeza Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo kwa kuifungua nchi kwa vitendo.

“Ushindi wa Dk Ndugulile kwa watu ambao ni wachambuzi wa diplomasia sio tu ushindi wa Dk Ndugulile, ni ushindi wa diplomasia ya Tanzania na sehemu ya utekelezaji wa falsafa yako (Rais Samia),” amesema Profesa Kitila.

Amesema ushindi wa Dk Ndugulile umetanguliwa na ushindi wa Dk Tulia Ackson kuwa Rais wa Mabunge ya Dunia (IPU).

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ambaye kabla ya uteuzi wake kutenguliwa Julai 21, 2024 na nafasi yake kuteuliwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alishiriki kwenye kampeni za kinyang’anyiro hicho.

Katika kurasa zake za kijamii, January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) ameelezea mambo manne yaliyochagiza ushindi huo wa Dk Ndugulile anayekwenda kuongoza nafasi hiyo na kuwa mtu wa kwanza wa ukanda wa Afrika Mashariki kushika wadhifa huo.

“Hongera Dk Ndugulile kwa ushindi ulioiletea heshima nchi yetu. Mambo manne yametubeba; sifa na uwezo wako binafsi, sapoti kubwa ya Rais na Serikali, heshima ya Tanzania Barani Afrika na kampeni mahiri. Pongezi kwa wote walioshiriki kampeni. Tunakutakia kila la heri.”

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameandika; “Hongera kwa kuchaguliwa, hongera kwa timu ya kampeni ya Tanzania. Kipekee, pongezi nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyowezesha kwa hali na mali kutafuta ushindi wa Dk Ndugulile.

“Ushindi huu ni fursa na heshima kubwa kwa nchi yetu. Tanzania imeshinda, Afrika imeshinda,” ameandika Ummy mtandaoni.

Hata hivyo, maswali yanayoulizwa na wengi ni kuhusu ukomo wa ubunge wake. Hata hivyo suala hilo liliwahi kuzungumzwa na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje, Makamba siku wakizindua kampeni hizo Mei 2024 alisema; “Kigamboni watakukosa, lakini Afrika watapata jembe. Dk Ndugulile ametumika hapa nchini na sasa anakwenda kutumikia nafasi nyingine iwapo kura zitaamua.”

Kauli ya Makamba ingawa hakuifafanua yeye mwenyewe na hata swali lilipoulizwa iwapo atashinda nafasi hiyo kama kuna uwezekano wa kuendelea na ubunge, inaashiria jimbo hilo litakuwa wazi na kuruhusu mgombea mwingine katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amempongeza Dk Ndugulile kwa kuchaguliwa na kuwapongeza washiriki wengine, akiwemo Sambo, Fall na Mihigo kwa kampeni zao.

“Dk Ndugulile amepata imani kwa nchi wanachama wa ukanda huu kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ajaye wa WHO Afrika. Hii ni fursa kubwa na jukumu kubwa sana.

“Mimi na familia nzima ya WHO barani Afrika na duniani kote tutakuunga mkono kila hatua,” amesema Ghebreyesus.

Walioshika nyadhifa kimataifa

Dk Ndugulile anakua miongoni mwa Watanzania kadhaa waliofanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali kimataifa, akiwemo Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson aliyechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Oktoba 27, 2023 katika uchaguzi uliofanyika Jijini Luanda nchini Angola.

Mwingine ni Dk Asha Rose Migiro, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi. Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Stephen Masele, aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Bunge la Afrika (PAP).

Related Posts