Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa amri na maelekezo kwa wajibu maombi akiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kufanya uchunguzi kuhusu mahali walipo viongozi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) na dereva wa pikipiki waliotoweka tangu Agosti 18, 2024.
Viongozi hao, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka, Katibu wake, Jacob Mlay na dereva wa pikipiki, Frank Mbise mpaka leo haijulikani mahali waliko.
Uamuzi huo wa Mahakama umetolewa leo Agosti 28, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera aliyesikiliza shauri la waombaji jana Jumanne, Agosti 27 ambao kupitia mawakili wao waliomba kabla ya kusikilizwa shauri lao la msingi, Mahakama itoe amri waachiwe kwa dhamana au iwaamuru wajibu maombi wawafikishe mahakamani wasikilize shauri lao.
Katika shauri hilo la maombi mchanganyiko ya Jinai namba 23998, wajibu maombi ni IGP, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO).
Wengine ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Temeke (OC- CID), Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe (OCS), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Jaji Dyansobera akitoa uamuzi amesema anatumia mamlaka ya kikanuni aliyonayo katika kutoa nafuu nyinginezo kama waombaji walivyoomba kuwa Mahakama itoe nafuu nyingine itakazoona zinafaa.
“Kwa kuzingatia hivyo viwili maombi mengine na mamlaka ya Mahakama chini ya Kanuni ya 12 za mwaka 1930 inatoa amri maelekezo hasa wajibu maombi wa kwanza mpaka wa tano kufanya uchunguzi kuhusu mahali walipo hawa waombaji,” ameamuru Jaji Dyansobera.
Hata hivyo, amesema aliyosema ni wajibu wa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa Sheria ya CPA, Sheria ya Jeshi la Polisi, Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO), Katiba ya nchi na sheria za kimataifa, kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Kwa hiyo Polisi watekeleze huo wajibu wa kupeleleza waliko hawa waombaji watatu. Kwa hiyo, maombi ya waombaji yanakubaliwa katika utaratibu nilioutaja,” amesema.
Mbali ya uamuzi huo, Mahakama imeamua kuwa hakuna ushahidi kuthibitisha kuwa waombaji wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kama ambavyo inadaiwa.
Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wanaamini waombaji walikamatwa na maofisa wa Jeshi la Polisi wa Kituo cha Polisi Chang’ombe, Mkoa wa Kipolisi Temeke.
Mawakili wa waombaji Deogratius Mahinyila na Paul Kisabo, wakiongozwa na Peter Madeleka walifungua shauri hilo la maombi mchanganyiko wakiomba kabla ya kusikilizwa kwa shauri hilo Mahakama itoe amri waachiwe kwa dhamana au iwaamuru wajibu maombi wawafikishe mahakamani wasikilize shauri hilo.
“Tunaomba Mahakama itoe amri waleta maombi waletwe mahakamani kwanza kwa mujibu wa kifungu cha 390 (1) (a) na (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)” alisema Madeleka wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo.
Alisema vifungu hivyo vinataka waleta maombi kwanza wafikishwe mahakamani ndipo taratibu nyingine ziendelee.
Wakili Kisabo alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Mashauri la maombi ya aina hiyo (watuhumiwa waliowekwa kuzuizini kuachiwa huru au kufikishwa mahakamani – Habeas Corpus), Mahakama ina mamlaka ya kutoa dhamana wakati wakisubiri usikilizwaji wa shauri lao.
Wakili Kisabo alisema Kanuni ya 12 inaipa mamlaka mahakama kutoa amri kwa wajibu maombi kuwafikisha waombaji mahakamani na kwamba, yote hayo yanafanyika kabla ya shauri kusikilizwa.
Mawakili wa Serikali, Monica Ndakidemi na Cuthbert Mbilinyi walipinga maombi hayo wakidai mawakili wa waombaji hawana uhakika na hawajawasilisha ushahidi kuwa waombaji hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Walidai walifuatilia Kituo cha Polisi Chang’ombe wakaelezwa hawapo mahali hapo, akiahidi kuendelea kufuatilia zaidi.
Katika uamuzi, Jaji Dyansobera amesema baada ya kuzingatia kwa umakini kiapo kinachounga mkono maombi hayo, ambacho ni ushahidi wa hoja za mawakili wa waombaji, Mahakama imeridhika hakuna uthibitisho wa kutosha kwamba waombaji wako chini ya mamlaka ya wajibu maombi.
Jaji Dyansobera amerejea kusoma aya zote za kiapo cha Mohamed H. Mzindu, ambaye amejitambulisha kama rafiki wa waombaji hao.
Jaji Dyansobera amesema maelezo yaliyomo kwenye aya ya tano mpaka ya 11 za kiapo hicho hayathibitishi kuwa waombaji wako katika himaya ya Polisi.
“Kwa hiyo kwa hayo ambayo tumeyasikia kutoka kwenye kiapo ambayo ndiyo ushahidi hakuna maelezo kutoka kwa muapaji kwamba alishuhudia wakiwekwa kizuizini na Polisi.”
“Kwa misingi hiyo Mahakama inasita kutumia kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Kanuni ya 12 ya maombi ya Habeas Corpus za mwaka 1930, kuamua kwamba waombaji waletwe mahakamani,” amesema.
Hata hivyo, amesema katika aya ya tano mpaka ya tisa, kuna tuhuma ambazo Mahakama haiwezi ikazipuuza maana ni kubwa zinagusa kutoweka kwa raia (waombaji) bila maelezo yoyote, jambo ambalo ni hoja ya jamii.