Mtoto amponza mama yake mzazi, afungwa jela miezi sita

Mbulu. Mkazi wa Kijiji cha Moringe, Kata ya Daudi mkoani Manyara, Anna Burra amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Mbulu kutumikia kifungo cha miezi sita jela baada ya kushindwa kumfikisha mahakamani mshtakiwa Carol Christopher (18), anayekabiliwa na shtaka la kumlawiti mtoto mwenye wa miaka miwili na miezi tisa.

Awali, Anna alikuwa amemdhamini Carol ambaye ni mtoto wake wa kumzaa kwa dhamana ya Sh3 milioni katika kipindi chote cha mwenendo wa shauri hilo.

Leo Jumatano Agosti 28, 2024, Mahakama ya Wilaya ya Mbulu imehukumu Anna kifungo cha miezi sita, hii ikiwa ni tarehe rasmi ya kutoa hukumu kulingana na mwenendo mzima wa shtaka.

Hukumu hiyo imetokana na Anna kama mdhamini, kuieleza mahakama mara kadhaa kuwa Carol hakuweza kufika mahakamani kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na tumbo la kuhara na kulazimika kwenda mkoani Arusha kwa matibabu katika Hospitali ya Seliani.

Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Mwendesha mashtaka, Maraba Masheku umeridhia ombi la Anna mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Johari Kijuwile huku ulimwamuru afike mahakamani hap oleo na mshtakiwa Carol pamoja na vielelezo vinavyothibitisha kulazwa kwake katika hospitali ya Seliani, lakini Anna ameshindwa kutekeleza agizo hilo.

Leo akiwa na mtoto mgongoni, Anna amefika mahakamani hapo na alipohojiwa na upande wa Jamhuri, amesema kuwa Carol hapatikani kwa simu na hajui sababu ya kutopatikana kwake. Kutokana na majibu hayo, Masheku akaiomba Mahakama kutoa hukumu dhidi ya Anna kwa kudanganya mahakama na kushindwa kuwasilisha vielelezo alivyotakiwa.

Masheku pia akaiomba mahakama kuwasilisha dhamana ya Sh3 milioni na kufuatia kifungu cha 160(4) cha Sheria ya Mwaka 2022.

Akisoma hukumu, Hakimu Kijuwile aliridhia ombi hilo na kutoa adhabu ya kifungo cha miezi sita kwa Anna kutokana na kushindwa kumfikisha mshtakiwa mahakamani na kushindwa kulipa Sh3 milioni.

Pia, Hakimu Kijuwile alitoa amri ya kukamatwa kwa Carol Christopher baada ya hukumu kutolewa.

Hata hivyo, nje ya mahakama, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walishangazwa na uamuzi huo, wakisema kuwa hawakujua kwamba mdhamini anaweza kufungwa ikiwa atashindwa kumfikisha mshtakiwa mahakamani.

Elizabeth Bilauri, mkazi wa Kata ya Daudi, alisema kuwa hukumu hiyo imekuwa funzo kwa jamii, akieleza: “Huyu mama alimdhamini mtoto wake kwenye hiyo mahakama ila hakumfikisha, ndiyo maana akahukumiwa kifungo, ila akilipa Sh3 milioni ataachiwa.”

Related Posts