Serikali yatoa majibu adhabu ya kifo, kukazia hukumu

Dodoma. Wakati Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Serikali imesema suala la kukazia hukumu na adhabu ya kifo ni vitu ambavyo vinafanyiwa kazi, na mabadiliko ya baadhi ya sheria yameanza kuonekana.

Pia, imesema Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 imeendelea kufanyiwa kazi kwa kukusanywa maoni na itakapokamilika itawasilishwa bungeni.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 29, 2024 wakati wa majumuisho ya hoja zilizotolewa na wabunge waliochangia mjadala wa mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wizara imeliomba Bunge na likaidhinisha Sh441.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, huku ikiwa na vipaumbele 15.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi amejibu hoja kadhaa zikiwamo za kukazia hukumu, mlolongo wa kesi na adhabu ya kifo.

Jaji Feleshi amesema kuna maeneo Serikali imeyafanyia kazi.

“Kwa mfano, kwa sasa mtu anayepeleka shauri Mahakama ya Rufani hahitaji kuomba kibali,” amesema.

Amesema jitihada zingine ambazo zimefanyika ni kupunguza milolongo ya upatikanaji wa nyaraka za mahakama, kwamba sasa inapatikana kwa muda mfupi, tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kuhusu nakala halisi kubaki mahakamani na kumfanya mtu kushindwa kutumia nyaraka zake kufanya mambo mengine, amesema inawezekana mtu kuacha nakala iliyothibitishwa na kuchukua halisi kwa ajili ya kufanyia mambo yake mengine.

Jaji Feleshi akizungumzia hoja kuhusu wafugaji walioshinda kesi mahakamani na kushindwa kurejeshewa mifugo yao kwa muda mrefu, amesema suala hilo linashughulikiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na taasisi zingine na kwamba Mei 2, litafika mwisho.

Akizungumzia hoja ya mifugo kutokurejeshwa hata baada ya kushinda kesi, amesema Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau wengine, wanalifanyia kazi na wako kwenye hatua ya kufikia mwisho.

Hoja ya kuchelewa kesi za mauaji na watu kukaa muda mrefu magerezani, wakiwamo waliohukumiwa adhabu ya kifo kukaa bila kutekelezwa adhabu hiyo, amesema baada ya Rais (Samia Suluhu Hassan) kupokea taarifa ya haki jinai Julai 15, 2023, jambo hilo lilikuwa ni miongoni mwa yaliyofanyiwa uchunguzi.

Amesema taarifa hiyo ina mapendekezo ya hatima ya watu wenye vifungo vya maisha na ya watu ambao wana hukumu za kunyongwa (hukumu za kifo) na hazijatekelezwa.

“Taarifa ile ilikuwa na mapendekezo ambayo sasa yanafanyiwa kazi kuangalia namna ya kubadilisha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kwa upande wa adhabu ya maisha kuwe na vigezo vingine isiwe tu kifungo cha maisha.”

“Kwa upande wa adhabu ya kifo kuna mapendekezo yalitolewa kwamba mahakama isifungwe mikono, jaji anayesikiliza au mahakama inayosikiliza iweze kutoa adhabu nyingine kutokana na mazingira,” amesema.

Jaji Feleshi amesema: “Kwa hiyo mabadiliko ya sheria lazima yatakuja bungeni. Pia, mimi AG, mkurugenzi wamashitaka na ofisi zingine tunayo dhamana ya kushughulikia lalamiko la mtu mmoja mmoja ambalo linakuwa na mazingira ya kipekee. Kinachohitajika ni kupewa lalamiko ambalo linakuwa rahisi kulifuatilia.”

“Tumekuwa tukifanya hivyo mara nyingi ikiwamo kukagua magerezani na kufanya vikao na vyombo vinavyofanya uchunguzi,” amesema.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana akijibu hoja kuhusu Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 amesema iliwahi kupelekwa bungeni.

“Umri wa kuoa au kuolewa uwe miaka 18, sheria hii ilishakuja bungeni kupitia tangazo la Februari 2021. Sheria hii ilipofika bungeni waliekeza tuende tukakusanye maoni.”

“Tumekusanya maoni na tunaendelea kukusanya maoni. Hapa kuna mawazo tofauti wapo wanaoafiki watoto wasiolewe kabla ya miaka 18, wapo wanaotaka kuliangalia kwamba hata akiolewa anaweza kurudi shule,” amesema.

Mapema katika michango yao, baadhi ya wabunge wametaka utaratibu wa kukazia hukumu mtu anaposhinda kesi uangaliwe upya, kwa kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni.

Wabunge Mashimba Ndaki wa Maswa Magharibi na Edward Ole Lekaita wa Kiteto wametaka Serikali ibadilishe sheria ya kukazia hukumu wakieleza ni mlolongo mrefu na badala yake mtu anaposhinda kesi akabidhiwe haki yake bila kuchelewa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond ameshangaa kwa nini adhabu ya kifo haitekelezwi, na kama Serikali haiitaki ni vema ikapeleka muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni, ikaondolewa.

Related Posts