Aliyeshiriki kuchanganya udongo wa Muungano afariki dunia, Rais Mwinyi aongoza mazishi.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewaongoza viongozi na wananchi katika mazishi ya Omar Hassan Mkele (76), mmoja kati ya watu waliobeba na kuchanganya udongo wa pande mbili za Muungano mwaka 1964.

Omar amefariki leo Jumatano na mazishi yamefanyika leo, Kibweni Uwanja wa Mpira nje kidogo ya Mji wa Unguja.

Sherehe za kuchanganya udongo wa pande mbili uliowekwa kwenye vibuyu viwili tofauti zilifanyika Aprili 26, 1964 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dare es Salaam na Mwalimu Julius Nyerere alichanganya udongo kwa kuumimina ndani ya chungu kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mapema Dk Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya maiti katika Msikikti wa Kibweni Mshelishelini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi. 

Baada ya maziko, Dk Mwinyi alifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji na kuwapa pole wafiwa na kuwataka kuwa na subira wakati huu wa msiba huo mzito.

Viongozi mbalimbali wameshiriki maziko hayo akiwemo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk, Mohd  Said Dimwa.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Ali Suleiman Ameir Mrembo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma.

Related Posts