RAMADHAN Elias ambaye ni mdau wa michezo, amesema ishu kubwa ambayo inazitesa timu za Tanzania katika michuano ya kimataifa ni kutokuwa tayari.
Elias ameyabainisha hayo leo Agosti 28, 2024 wakati akichangia mada katika Mwananchi Space, inayoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) isemayo: “Tumekosea wapi timu nne za Tanzania kutolewa mashindano ya klabu Afrika?”
Mdau huyo amesema ukiangalia timu nne za Tanzania Bara ambazo zimekuwa zikipata nafasi ya uwakilishi wa nchi kimataifa zimekuwa zikienda kutokana na kanuni inavyotaka, lakini hazipo tayari kwa mashindano hayo.
Akitolea mfano wa wawakilishi waliowahi kutolewa mapema, ameitaja KMC ambayo ilipopata nafasi hiyo haikutoboa wakati Biashara United ilishindwa hadi kusafiri kwenda kucheza mchezo wa marudiano ugenini.
“Tulikopita hata kwa Geita Gold ilitolewa hatua kama hiyo na safai hii imekuwa kwa Azam na Coastal Union, mbali na JKU na Uhamiaji,” amesema Elias
Ameongeza kwamba kwa kuwa Tanzania Bara ina nafasi ya kupeleka timu nne kimataifa, mbali na Simba na Yanga, timu zingine zimekuwa zikipambana angalau zimalize nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ili kuona namna ya kupata nafasi hiyo, tukitofautiana na klabu za nchi za Morocco au Misri.
Ushauri wake ni kwamba, timu zilizobaki Simba na Yanga ziendelee kupambania Tanzania kubakisha wawakilishi wanne, kisha wengine wajifunze lakini pia wadhamini wanapaswa kujitokeza kwa wingi.