MDAU wa soka nchini, Hosea Gambo Paul ‘Gambo Jr’ amesema kama kuna sehemu Azam FC ilikosea ni vyema ikaenda kuomba msamaha kutokana na kushindwa kufanya vyema katika michuano ya kimataifa, kwani ni klabu iliyokamilika kwa kila kitu.
Gambo ameyabainisha hayo leo Agosti 28, 2024 wakati anachangia mada kwenye mjadala unaoendeshwa na Mwananchi X Space unaohoji ‘Tumekosea wapi timu nne za Tanzania kutolewa mashindano ya klabu Afrika’ inayoendelea kwa sasa akisema kwa klabu za Zanzibar kunaweza kuwa na sababu ikiwamo uwekezaji mdogo.
Amesema kutolewa kwa JKU na Uhamiaji inaweza kuwa na mashiko, lakini kwa Azam FC inashangaza kwani ina kila kitu kuanzia benchi la ufundi na wachezaji, huku akisema kwa Coastal Union iliyotolewa Kombe la Shirikisho inatokana na kuangushwa na uzoefu na kupoteza ugenini kwa mabao 3-0.
“Coastal ina matatizo mengi ina mizozo na wachezaji wake, lakini kwa hawa Azam kama kuna sehemu walikosea ni vyema wakaenda kuomba radhi kwa hali inayowakuta,” alisema Gambo Jr.