Majeruhi ajali ya treni wasimulia ilivyotokea

Kigoma. Majeruhi wanne kati ya watano  wa ajali ya treni iliyotokea mapema leo, wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Maweni kwa matibabu zaidi.

Majeruhi hao walikuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Uvinza kabla ya baadhi kuhamishiwa Hospitali ya Maweni kwa matibabu zaidi.

Awali, taarifa iliyotolewa kwa umma na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Jamila Mbarouk ilisema ajali hiyo imetokea leo Jumatano Agosti 28, 2024 kati ya stesheni ya Kazuramimba na Uvinza na watu 70 wamejeruhiwa katika ajali.

Treni hiyo ilibeba abiria 571 waliokuwa wakisafiri kutokea mkoani Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Wakizungumza na Mwananchi Digital wakati wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni baadhi ya majeruhi wamesema wakati ajali hiyo inatokea na mabehewa kuanguka walikuwa wamelala.

Majeruhi Zena Faresi (45) amesema walianza safari yao jana usiku muda wa saa tatu usiku, kuelekea jijini Dar es Salaam na wakati ajali inatokea alikuwa amelala hakuweza kuona kilichotokea alishtukia yupo chini na akapoteza fahamu wakati huohuo hivyo hakujua nini kiliendelea.

“Niliposhtuka usingizi nilijikuta niko chini naambiwa ilikuwa saa nane usiku, wakati najaribu kujiokoa nikapoteza fahamu na kwa sasa nasikia maumivu sehemu ya mkono wa kushoto,”amesema Feresi.

Majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Yusta Ezekiel (21) amesema alikuwa amelala na hakujua kinachoendelea wakati ajali inatokea ameshtuka akiwa na maumivu makali ya mkono ambao ulikandamizwa na kioo.

“Nilipokuwa najitahidi kuutoa nikagundua kuwa nimevunjika, nikaomba msaada kwa watu wengine wakanifunga na miti wakakaza na Kamba na baadaye tukasafirishwa kupelekwa Hospitali ya Wilaya Uvinza, ila kwa sababu nimevunjika nikapewa rufaa kuja hapa Maweni kwa matiabu zaidi,” amesimulia Ezekiel.

Hata hivyo amesema bado ana maumivu sehemu za maungio ya mkono lakini tayari ameshachukuliwa vipimo anasubiri majibu.

Abiria mwingine aliyejeruhiwa, Hamida Hamza (37) amesema wakati wametoka Stesheni ya Kazuramimba treni hiyo ilikuwa ikitembea mwendo kasi kiasi cha kuwatia shaka.

“Nilikuwa nazungumza na wenzangu lakini kabla ya kuanguka tukasema mbona treni inakimbia sana, kila mtu akawa na hofu,” amesimulia abiria huyo.

Hamza anasema haukupita muda, akapitiwa na usingizi alizinduka alijikuta yuko chini alipokuwa anajitahidi kujiokoa akapoteza fahamu amekuja kuzinduka akiwa Hospitali ya Maweni.

Amesema ana maumivu sehemu ya mgongo, kifua na kwenye mbavu na alikuwa anasubiri  kuingia kwenye vipimo.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Lameck Mdengo amesema wamepokea majeruhi watano kutoka Hospitali ya Wilaya Uvinza, mmoja ameshapata vipimo na kuruhusiwa na wanne wanaendelea kupata matibabu ya kibingwa hospitalini hapo.

Amesema kati ya majeruhi hao wanne ni wanawake na mwanaume mmoja ambaye ana majeraha zaidi.

Amesema majeruhi huyo amevunjika mgongo na alikuwa anasubiri kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.

Dk Mdengo amesema majeruhi wengine wanane waliokuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Uvinza wanaendelea na matibabu.

Related Posts