MKURUGENZI wa Fedha na Mipango wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Awadh Maulid Mwita amewataka Azam FC kuongeza wigo wa mashabiki wa timu yao ili ipate presha ya kusaka matokeo chanya kwenye mechi zao.
Mwita ameyabainisha hayo leo Agosti 28, 2024 wakati akichangia kwenye mjadala wa Mwananchi Space, inayoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) wenye mada isemayo; Tumekosea wapi timu nne za Tanzania kutolewa mashindano ya klabu Afrika?
Mwita amesema Azam FC ina karibu kila kitu katika timu hiyo kinachohitajika ili iweze kuwa timu bora, lakini imeshindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji wake kukosa presha ya kutakiwa kufanya vizuri.
Mwita amesema klabu zingine za Simba na Yanga zinakutana na presha kubwa ya mashabiki wao pale wanapokosa matokeo mazuri hatua ambayo inawafanya viongozi na wachezaji kujituma na kupata matokeo mazuri.
Akizungumzia timu za Zanzibar ambazo nazo zimetolewa mapema zikiwamo JKU na Uhamiaji, Mwita amesema tatizo linalozikwamisha timu hizo ni ukosefu wa fedha ambapo ametaka wawekezaji kuendelea kujitokeza kuokoa jahazi.