Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema chama hicho, kinakubaliana na uamuzi wa Jeshi la Polisi lililozuia mkutano uliopangwa kufanyika wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.
Leo Jumatano Agosti 28, 2024 katika mitandao ya kijamii ilisambaa barua iliyoandikwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro, L. Ncheyeki kwenda CCM ikieleza kutokana na shughuli za kuimarisha usalama zinazoendelea katika maeneo ambayo CCM wameomba kufanya mikutano Ngorongoro, Jeshi hilo limesitisha mikusanyiko hadi watakapoelekeza vingine.
Katika maelezo yake, Makalla amesema CCM ina heshimu utaratibu wa sheria na wanatii hatua hiyo ya Jeshi Polisi iliyozuia mikutano hiyo iliyopangwa kufanyika Septemba katika ziara ya kuimarisha chama hicho wilayani Ngorongoro.
“Chama chetu kinaheshimu kanuni na taratibu na mkutano wangu umekataliwa,” amesema Makalla.
Amesema hayo leo Jumatano Agosti 28, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Azimio wilayani Temeke akiwa ziarani mkoani Dar es Salaam.
Makalla amesema hayo akijenga hoja ya kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda kupanda jukwaani na kuwaita watendaji kujibu kero za wananchi ili kuendana na muda kabla ya saa 12.00 ambayo ni mwisho wa mkutano huo wa hadhara.
Mbali na CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini ni miongoni mwa vyama vilivyopanga kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Ngorongoro kwa lengo la kuzungumza na wananchi.
Hatua ya Chadema ilichangiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuendelea na taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kutokana na uamuzi wa Mahakama kuzuia tamko la Serikali la kufuta kata vijiji na vitongoji vya wilaya hiyo.
Mikutano ya Chadema pia imezuiwa na polisi.