Wazawa wasipobadilika wataendelea kulalamika -SMZ

Unguja. Wakati asilimia 60.6 ya shughuli za utalii Zanzibar zikielezwa kufanywa na wageni, Serikali imesema iwapo wazawa wasipobadilika wataendelea kulalamika nafasi hizo kuchukuliwa na watu kutoka nje ya nchi.

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Zena Said amesema hayo leo Agosti 28, 2024 alipofungua semina ya makatibu wakuu wa SMZ na wadau wengine walipo kwenye mnyororo wa utalii kuhusu utalii endelevu.

Amesema lazima kuangalia matakwa ya sekta hiyo, hivyo watengeneze vijana waweze kukidhi.

“Sasa hizi jeuri tulizonazo ambazo tunatoleana huku ukienda ukatoa kule, wale watalii wanaripoti na mwenye hoteli hawezi kukubali akose wateja kisa unawatolea wateja wake jeuri, atakufukuza tu,” amesema.

“Kwa hiyo lazima tujue nini kinatakiwa halafu na sisi tuanze kubadilika, tusipobadilika siku zote tutalalamika, na sisi hatuwezi kulazimisha aweze kuajiri vijana ambao hawana sifa kwa hiyo sifa zile tukubali tuzipate tuweze kuajirika na mwishowe tutakuwa tunachukuliwa Wazanzibari,” amesema.

Zena amesema hiyo siyo kazi ya Serikali pekee lazima kuwe na utayari wa vijana kufanya kazi na kuwa na haiba na sifa zinazotakiwa katika sekta hiyo inayohitaji ukarimu wa hali ya juu.

Akizungumzia utalii endelelevu, Zena amesema Serikali inatamani sekta ya utalii iendelee kuchangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi wa Taifa lakini usiharibu mazingira, utamaduni na mila za Taifa hilo.

Amesema wakati wanahamasisha utalii ipo haja ya kuufanya katika njia endelevu bila kuathiri masuala ya kijamii na kimazingira.

“Lazima sisi tuone kama juhudu tunazofanya zinatupeleka katika utalii huo na kama nchi mwelekeo wetu uweje katika uwekezaji sekta ya utalii uweje,” amesema

Amesema wameshakubaliana mambo ya kufanya kwa sababu wanataka kulinda mazingira, mila na desturi za eneo husika wakati huohuo utalii ukileta faida kubwa za kiuchumi iwe sehemu ya kushauri wizara na Rais cha kufanya kuhusu utalii endelevu.

Amesema mipango ya Serikali ipo mingi kuhakikisha utalii unaongezeka mbali na utaii wa fukwe lakini kwa sasa wapo kwenye mpango wa kujenga kumbi za mikutano na kupanua sekta ya afya watu wavutike kutibiwa.

“Tunataka utalii wa mikutano pamoja na maonyesho uongeze pato la Taifa lakini kwenye kuelekea hilo, watu waje kwa wingi tupate faida za kiuchumi na tusipate athari za kijamii na kimazingira,” amesema.

Amesema wakati mwingine nchi inaweza ikawa haijakidhi vigezo vya utalii endelevu lakini ikawa na hoteli ambazo zimekidhi vigezo kwa hiyo nchi inaweza kupata hati ya utalii endelevu.

Akitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya utalii, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Fatma Mbarouk Khamis amesema asilimia 60.6 ya shughuli zote za utalii zinafanywa na wageni.

Amesema asilimia 80 ya taka zinazozalishwa Zanzibar zinatokana na sekta hiyo. Hata hivyo, amesema jambo hilo linaweza kuwa fursa kwa upande mwingine kuzitumia katika kurejerea na kuzalisha bidhaa zingine.

Amesema kuna masuala ya utamaduni na asili yanaharibika na hakuna mfumo mzuri kati ya sekta binafsi na Serikali kwani hawaongei lugha moja.

“Boti zinazokwenda kuona utalii wa Dolphine ni nyingi kwa hiyo hakuna utaratibu mzuri na jambo hilo linasababisha kuvuruga eneo hilo, huku dhana ya utalii kwa wote nayo bado haijaeleweka,” amesema.

Amesema utafiti unaoyesha asilimia 80 ya watalii wote duniani wanapendelea zaidi utalii endelevu, hivyo ipo haja na Zanzibar kuwa na utalii wa namna hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk Aboud Jumbe amesema semina hiyo ya siku moja itasaidia wasimamizi na watuga sera kuona namna ambavyo wanaweza kuweka mipango inayendana na utalii endelevu.

“Hii itasaidia kuangalia vpaumbele vya Serikali kuoanisha na utalii wetu kwa hiyo zitaongezwa programu na kusaidia kutayarisha sera jumuishi,” amesema.

Related Posts