Michezo ya Olimpiki kwa wenye Ulemavu yafungua pazia Paris – DW – 29.08.2024

Sherehe hizo za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki kwa wanariadha wanaoishi na Ulemavu zilifanyika katikati mwa mji mkuu wa Ufaransa, Paris huku kukiwa na nyimbo na mambo mbalimbali ya kupendeza.

Kama ilivyokuwa kwa sherehe ya ufunguzi wa Olimpiki kwenye Mto Seine mnamo mwezi Julai, sherehe hizo zilifanyika mbali na uwanja mkuu utakaoshuhudia mashindano hayo kwa siku 11 mfululizo.

Hali ya hewa ilikuwa tulivu, tofauti na mvua kubwa iliyonyesha wakati wa kufunguliwa kwa  Michezo ya Olimpiki ya msimu wa Joto. Sherehe hizo zilifunguliwa katika eneo maarufu mjini Paris linalojulikana kama Place de la Concorde.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer pamoja na watu maarufu kuanzia wasanii kutoka Canada pamoja na  wanamichezo mbalimbali.

Jumla ya wanariadha 4,000 kuhudhuria

Mwanariadha mwenye ulemavu wa Ujerumani Johannes Floors akiwa jijini Paris.
Mwanariadha mwenye ulemavu wa Ujerumani Johannes Floors akiwa kwenye mazoezi jijini Paris.Picha: Mika Volkmann/picture alliance

Wanariadha 4,400 kutoka mataifa 168 walishuka kwenye barabara inayopakana na mtaa maarufu wa Champs-Elysees mbele ya maelfu ya watazamaji wanaokadiriwa kufikia 50,000.

Wanariadha wenye ulemavu wa kimwili, viungo kama macho na hata matatizo ya kiakili watashindana katika jumla ya michezo 22 kuanzia leo Alhamisi hadi Septemba 8.

Jumla ya viwanja 18 kati ya 35 vya  Olimpiki  vitatumiwa pia kwenye Michezo ya Olimpiki ya watu wanaoishi na ulemavu ikijumuisha viwanja vya Grand Palais na Stade de France.

China, yenye kikosi chenye nguvu katika michuano hii ya Olimpiki kwa watu wanaoishi na ulemavu ilituma wanariadha mahiri. Katika michuano ya mjini Tokyo, China iliondoka na jumla ya medali 96 za dhahabu.

Zaidi ya tiketi milioni mbili zauzwa

Kiwanja cha Michezo ya Olimpiki kwa wenye Ulemavu mjini Paris
Kiwanja cha Michezo ya Olimpiki kwa wenye Ulemavu mjini ParisPicha: Ezra Shaw/Getty Images

Waandaaji wamesema zaidi ya tiketi milioni mbili tayari zimekwishanunuliwa huku kumbi zitakazopokea michezo kadhaa zikitangaza kuwa tayari nafasi zote tayari zimechukuliwa. 

Hata hivyo baadhi ya watu wamekosoa kitendo cha kufanyika michezo hiyo katika jiji ambalo mfumo wa usafiri haswa treni za chini, haujakidhi kabisa mahitaji kwa watu wanaotumia viti vya magurudumu, jambo ambalo wamesema watapata shida ya usafiri.

Mitandao ya kijamii ya Youtube na TikTok watakuwa washirika wa michezo hiyo. YouTube imetia saini ya ushirikiano na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu (IPC)  ili kupeperusha moja kwa moja mitandaoni michezo hiyo bila malipo hasa katika mataifa ya Asia, Amerika Kusini na Afrika, huku TikTok ikiwa inachapisha video kupitia kwenye kurasa maalum.

Matangazo hayo ya moja kwa moja yatakuwa yakipatikana katika nchi kama vile Algeria, Misri, Kenya, Indonesia, Chile, Colombia, Canada na Japan.

(Vyanzo: AFP, DPAE, Reuters, AP)

 

Related Posts