Sababu, faida bei ya Dhahabu kuvunja rekodi ya muda wote

Kuadimika kwa Dola za Marekani na kuwapo kwa uchaguzi nchini humo vimetajwa kuwa sababu za ongezeko ya bei ya dhahabu duniani hadi kufikia kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa.

Tovuti ya Trading Economy Jumatano wiki hii ilionyesha kuwa wakia moja ilinunuliwa kwa Dola za Marekani 2,523 (Sh6.85 milioni), kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa tangu mwaka 1970 mauzo ya dhahabu yalipoanza kurekodiwa katika tovuti hiyo.

Kuongezeka kwa mauzo haya ni fursa kwa nchi ambazo zinazalisha madini hayo kwani zitakuwa na uwezo wa kupata mapato mengi zaidi yanayotokana na mauzo hayo. Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo.

Mbali na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo nje ya nchi, pia itaisaidia nchi kupata kodi nyingi kutoka kampuni zinazohusika na mauzo hayo pamoja na mirabaha inayolipwa kwa Serikali.

Akizungumzia ongezeko hilo la bei, Mchambuzi wa uchumi nchini, Oscar Mkude anasema hali hiyo imesababishwa na kushuka kwa mahitaji ya Dola za Marekani duniani kote, uchaguzi katika taifa hilo kubwa huku kukiwa na mfumuko wa bei, kinyume na matarajio ya wengi.

“Ili kutunza thamani ya fedha zake, mataifa yanakwenda kununua dhahabu kulingana na kiwango cha fedha zake, baadaye zikitaka kubadilisha dhahabu kuwa fedha, itakuwa rahisi,” anasema Mkude.

Anasema utaratibu huo hutokea pale watu wanapohisi thamani ya fedha zao inashuka, huwa wanaenda kununua dhahabu, huku akitolea mfano wa kipindi cha Ugonjwa Virusi vya Korona (Uviko 19) dhahabu ilivyopanda bei.

“Sababu ya kufanya hivyo wengi walikuwa wanaamini kufungiwa ndani kulikuwa kunaathiri mwenendo wa uchumi katika maeneo mbalimbali duniani na wengi walianza kununua vitu vya thamani kama dhahabu,” anasema Mkude.

Loading...

Loading…

Mkude anasema kitendo cha wengi kununua madini hayo kilisababisha bei yake kuanza kupanda na mataifa yaliyokuwa yanaizalisha, yalijikuta yakianza kupata faida ikiwemo Tanzania.

“Kwa sasa dola ina ushawishi mkubwa katika uchumi wa mataifa mengi duniani na tumeanza kuona ikianza kuleta changamoto na uchaguzi wa Marekani umekuwa ukianza kuleta shida katika masoko ya hisa,” anasema.

Mkude amesema hali hiyo inasababisha wawekezaji wajanja kuanza kubadilisha mtazamo na kuanza kununua dhahabu ili kunusuru uchumi wao.

Kwa upande wake, mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo anasema watu kukimbilia kununua dhahabu ni kutokana na sababu za historia.

“Mwanzoni wakati wa vita vya kwanza na vya pili vya dunia watu walikuwa wanashika dhahabu lakini baada ya vita vile Marekani iliibuka kuwa Taifa lenye nguvu baada ya fedha yake kuimarika,” anasema.

Anasema mtindo huo umekuwa ukijirudia kila dola ya Marekani ikishuka, watu wanakimbilia kushika dhahabu na kuwa hata Marekani yenyewe imekuwa ikinunua dhahabu ili kuhuisha uchumi wao.

“Kutokana na hali hiyo Umoja wa nchi zinzochipukia kiuchumi (Brics), unafikiria kuanzisha utaratibu wa kununua vitu kwa kutumia fedha zake, mfano Urusi na India wameshakubaliana kutumia fedha zao,” anasema.

Profesa Kinyondo anasema yote hayo wanayafanya ili kuikimbia dola inayoonekana kusumbua uchumi wao, akitolea mfano Tanzania kipindi cha Serikali ya awamu ya tano dola moja ilikuwa inauzwa kwa Sh1,800 lakini kwa sasa inauzwa Sh2,700.

“Watu wanajiminya kupata kitu kilekile kwa fedha kubwa si kwa sababu kimepanda bei, bali kwa sababu watu wanaendesha dola lakini kunakuwa na vurugu,” anasema.

Ongezeko hilo la bei pia limekuwa neema kwa upande wa Tanzania kwani katika mwaka 2023 mauzo yaliyotokana na uuzaji wa madini hayo yaliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2022.

Kwa mujibu wa takwimu msingi za Tanzania zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mauzo ya dhahabu yalifikia Sh7.27 trilioni mwaka 2023 kutoka Sh6.49 trilioni mwaka uliotangulia.

Licha ya mauzo hayo kuongeza, uzalishaji wa madini hayo ulionekana kushuka kwa kiasi hadi kilo 54,760 mwaka 2023 kutoka kilo 56,943 mwaka uliotangulia.

Hata hivyo, hali hii haikuzuia kushuhudiwa kwa ongezeko la uzalishaji wa vito vitokanavyo na dhahabu na fedha, kwani ripoti hii inaonyesha kuwa uzalishaji wake ulifikia gramu 29,699 mwaka 2023 kutoka gramu 20,037 mwaka uliotangulia.

Mauzo haya yameendelea kushuhudiwa kupaa zaidi kwani ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi ya Julai, 2024 inaonyesha kuwa mauzo hayo yalifikia Sh8.47 trilioni Juni mwaka huu kutoka Sh7.89 trilioni mwaka uliotangulia.

Mauzo ya dhahabu yalibeba asilimia 49 ya mauzo yote ya bidhaa asili yaliyofanyika katika mwaka ulioishia Juni 2024 kwa mujibu wa BoT.

Mbali na mauzo haya, hata bajeti ya Wizara ya Madini iliyowasilishwa na Waziri Antony Mavunde inaonyesha kuwa mapato yaliyotokana na ‘Stamigold’ yaliongezeka.

Stamigold ni mgodi unayomilikiwa na Serikali kupitia Stamico inayomiliki hisa asilimia 99 na Ofisi ya Msajili wa Hazina inayomiliki hisa asilimia 1.

“Katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 mgodi umezalisha dhahabu wakia 7,449.60 na kupata Sh36.57 bilioni. Kiasi cha Sh1.46 trilioni kimelipwa Serikalini kama mrabaha na ushuru wa huduma na Sh914.48 milioni ikiwa ni ada ya usimamizi,” alisema Waziri alipokuwa akisoma bajeti.

Pia, kwa sasa mgodi umeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kupunguza gharama za nishati kwa wastani wa Sh700 milioni kwa mwezi.

Wakati bei yake ikizidi kupaa katika soko la kimataifa, kwa miaka 20 sasa Tanzania imekuwa ikiitegemea mauzo ya madini kama chanzo kikuu cha mapato ya nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/2025 iliyosomwa na Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, katika miaka 20 iliyopita Tanzania iliuza zaidi mazao ya kilimo wakati sasa mauzo ya nje yanatawaliwa zaidi na madini.

“Pia katika miaka 20 iliyopita tuliuza zaidi bidhaa zetu katika masoko ya Ulaya, Marekani na Afrika lakini kwa sasa tunauza zaidi katika masoko ya nchi za Asia (China, India), Kenya na Uganda na nchi za Mashariki ya Kati,” anasema Profesa Mkumbo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, katika miaka ya 2000, bidhaa zilizokuwa zikiuzwa sana ni dhahabu kwa asilimia 11.6, almasi (asilimia 7.47), Fish fillet (asilimia 13.9) nazi, Brazil nuts na korosho kwa asilimia 8.18, pamba ghafi (asilimia 4.48), tumbaku ghafi (asilimia 7.34) na kahawa kwa asilimia 9.22.

Tofauti na miaka ya kuanzia 2020 ambapo bidhaa zilibadilika na sasa dhahabu ilibeba asilimia 39.9 ya mauzo yote ya nje huku mazao ya nazi, Brazil nuts na korosho yaliyofuata kwa kuuzwa nje kwa wingiyakiwa na asilimia 6.52 pekee na mazao kama pamba, kahawa yakiwa chini ya asilimia nne kila moja.

Mtaalamu wa Uchumi, Dk Donath Olomi anasema anasema mara zote bei inapoongezeka kama nchi inaongeza kiwango cha mapato kinachopatikana kutokana na kodi inayolipwa na mirabaha.

Kodi hizo ni zile zinazolipwa na kampuni zinazojihusisha na uuzaji wa dhahabu kwani wanapopata faida kiwango chao cha kodi huongezeka sawa na bidhaa nyingine yoyote ikipanda.

“Nchi za wenzetu wenye bidhaa kama hizi wanapoona bei imepanda, kuna mfuko ambao wanaingizia fedha za faida zinazozidi, zinatunzwa huko kwa ajili ya kuzalisha bidhaa nyingine kwa nchi wakati ambao dhahabu au mafuta hayatakuwapo,’ anasema Dk Olomi.

Hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo haina mfumo huo na badala yake kinachoweza kufanyika ni kujazia pengo na kuimarisha sehemu ambazo zilikuwa zikionekana kulenga ikiwemo kuongeza fedha za kigeni.

Mkude anasema Serikali inapaswa kuwa na hifadhi ya kutosha ya dhahabu na kuuza pale soko linapochangamka, akimaanisha bei inapoongezeka.

“Nchi inapaswa kutengeneza mfumo wa kuongeza thamani ya ndani, tusiuze dhahabu ghafi lakini tukiongeza thamani wakati bei inapanda kule nje hata wale waliopo kwenye mchakato wa uchakataji ndani wananufaika,” anasema Mkude.

Anasema mfumo uliopo sasa nchini unabana kiasi kwamba wananufaika wale wanaochimba pekee, lakini baada ya mchakato huo kunakuwa na mwisho wa mzunguko.

“Lazima tuongeze mzunguko wa uchumi nje ya uchimbaji wa dhahabu, kwamba isiishie kwenye kuchimba. Kuwe na kitu kingine kinachofanyika ndani ya nchi na kuangalia aina nyingine za madini,” anasema.

Anasema changamoto iliyopo nchini ni kukosekana kiwanda cha kufanya uchakataji au uchenjuaji, suala ambalo limechukua mchakato mrefu kuanzisha wakatio kipindi cha awamu ya tano walikuwa wanafikiria kuanzisha.

“Nilipata taarifa baadhi ya makampuni yalikuwa yameanza kufikiria namna ya kuanzisha ingawa viwanda vyake vinahitaji umeme mkubwa ili kuweza kufanya hiyo kazi sasa kukawa na maswali mengi kwamba umeme uliopo si toshelevu,” anasema.

Anasema licha ya mjadala ni muhimu serikali kuweka nia kuangalia namna ya kufanya kwa kuanzisha kiwanda hicho kwa kufikiria kuongezea na umeme wa jua na upepo kwa ajili ya mradi.

“Kufanya hivyo kutaondoa hofu kwenye mfumo uliopo na kuendelea kuongeza fursa za ajira,” anasema.

Ili kuhakikisha madini yanaendelea kupatikana, moja ya malengo ya Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 ni Stamico kuendelea na utafutaji wa madini katika leseni zake ikiwemo leseni ya uchimbaji wa dhahabu katika eneo la Pida lililopo Mkoa wa Mara pamoja na leseni za madini mkakati na muhimu ya cobalt na nikeli – Kagera, shaba – Kilimanjaro, lithium – Dodoma, kinywe – Lindi na rare earth elements – Songwe.

Pia Shirika litaimarisha ufuatiliaji wa miradi ya ubia ambayo ni Mgodi wa Buckreef na Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza pamoja na Kampuni tanzu ya STAMIGOLD ili kuongeza ufanisi na kuwezesha ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye miradi hiyo.

Related Posts