Morogoro. Mradi wa utafiti wa kuongeza matumizi ya taarifa za bioanuai kwa uhifadhi endelevu na kipato kwenye milima ya tao la Mashariki nchini umebaini uwepo wa zaidi ya bioanuai 3,935 kwenye misitu ya asili ya hifadhi ya Kilombero, Udzungwa na Uluguru.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 29, 2024 mjini Morogoro na Mkuu wa mradi huo wa utafiti, Profesa Pantaleo Munishi kutoka Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa maofisa uhifadhi kutoka kwenye misitu hiyo mitatu ya asili iliyo kwenye safu za milima ya tao la mashariki.
Munishi amesema matokeo hayo ya utafiti yatasaidia wahifadhi kutambua na kuweka mikakati ya namna ya kutunza bioanuai hizo na kuzitangaza ulimwenguni ili kuongeza tija kwa Taifa.
“Milima ya Tao la Mashariki ni moja ya maeneo muhimu ya bioanuai yanayotambulika duniani na kupewa kipaumbele ili kutunzwa na kumekuwapo miradi mingi ya utunzaji wa misitu na bioanuai zilizomo, lakini kumekuwa hakuna taarifa sahihi za bioanuai zilizomo katika kipindi chote cha utekelezaji wa miradi hiyo,” amefafanua Profesa Munishi.
Amesema taarifa zilizopo pia hazipo sehemu moja kiasi cha kuwa rahisi kwa wahitaji kuzipata, hivyo kuchangia kupunguza jitihada za kuzitangaza lakini pia kuzihifadhi hasa katika kipindi hiki mabacho mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa makubwa na kusababisha kuathiri bioanuai nyingi na nyingine kupotea.
Mtafiti huyo mkuu amesema baada ya kukamilisha utafiti wao wa kuzitambua bioanui zinazopatikana kwenye misitu hiyo mitatu, wameamua kuwaita maofisa uhifadhi kutoka misitu hiyo na kuwapa taarifa lakini pia kuwafundisha namna bora za kutumia mifumo ya kimtandao kuzitangaza ili zifahamike duniani kote na kutunzwa.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, mkurugenzi mstaafu wa idara ya misitu na nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ezekiel Mwakalukwa amesema matokeo hayo mazuri ya utafiti yakitunzwa vizuri katika sehemu moja na kupatikana kirahisi, yatasaidia jamii na Serikali kufanya uamuzi sahihi ambao utaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Bioanuai ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa na mara nyingi kutokuwa na taarifa zake sahihi katika nchi au misitu kunapelekea uhifadhi wake kuwa mgumu na zingine kutoweka hivyo tafiti zinasaidia kuzitambua lakini kuweka mipango madhubuti ya kuzihifadhi ili ziendelee kutoa mchango stahiki kwenye maendeleo” ameeleza Dk Mwakalukwa.
Ofisa Mipango na Mawasiliano kutoka Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF), Alan Kimbita, ambao ndio wafadhili wa mradi huo, wamepongeza kazi iliyofanywa na watafiti hao kutoka SUA na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kuja na taarifa hizo muhimu zitakazowezesha kutambua bioanuai zilizopo kwenye maeneo hayo kwa sasa.
“Baada tu ya kuchapisha baadhi ya viumbe hai waliobainika kwenye misitu hiyo, tayari tumeanza kupata maswali kutoka maeneo mbalimbali duniani wakitaka kujua zinapopatikana na hii ni ishara njema kuwa kama taarifa zote zitakusanywa hivi na kutangazwa kikamilifu zitavutia wadau wengi kuja kuzitembelea kuziona na wengine kufanya tafiti na kusaidia uhifadhi,” amesema Kimbita.