Ujerumani yamtimua mkuu wa kituo cha Uislamu – DW – 29.08.2024

Mamlaka ya ndani ya Hamburg imetoa amri ya kurudishwa kwao Mohammad Hadi Mofatteh, 57, wiki hii kulingana na msemaji wa aliyetoa taarifa hiyo Alhamis. Hakutoa taarifa iwapo Mofatteh bado yupo nchini Ujerumani.

Barua hiyo inamtaka Mofatteh aihame Ujerumani ndani ya siku 14, la sivyo atarudishwa katika nchi aliyotokea kwa gharama yake mwenyewe. Kulingana na mamlaka hiyo, anastahili kuondoka Ujerumani ifikapo Septemba 11, 2024.

Fauka ya hayo, amepigwa marufuku ya kurudi Ujerumani au kuishi nchini humo na iwapo atafanya hivyo, huenda akafungwa jela kwa kipindi cha miaka mitatu.

Nguvu zote kutumiwa kupambana na itikadi kali

Mofatteh alikuwa mkuu wa IZH tangu kipindi cha majira ya joto mwaka 2018. Kulingana na utafiti wa shirika la kiintelijensia la Hamburg, ambalo rasmi linajulikana kama Afisi ya Taifa ya Kulinda Katiba, Mofatteh, alikuwa anachukuliwa kama mwakilishi rasmi wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei nchini Ujerumani, hadi hivi karibuni.

Kituo cha Kiislamu cha IZH mjini Hamburg, Ujerumani
Kituo cha Kiislamu cha IZH mjini Hamburg, UjerumaniPicha: Daniel Bockwoldt/dpa/picture alliance

Seneta wa zamani wa jimbo la Hamburg Andy Grote alisema kufukuzwa kwake kufuatia kupigwa marufuku kwa kituo hicho cha IZH, ndiyo hatua nyengine kubwa inayopigwa na mamlaka hiyo katika vita dhidi ya vitendo vya itikadi kali.

“Kama mwakilishi wa juu wa kidini wa utawala wa kinyama wa Tehran, muda wake Ujerumani umekwisha. Tutaendelea kupambana na itikadi kali za Kiislamu kwa nguvu zote na kutumia sheria zote za makaazi kufanya hivyo,” alisema Grote.

Mwishoni mwa mwaka 2022, makamu mkuu wa IZH. Seyed Mousavifar, alifukuzwa Ujerumani kutokana na mafungamano yake na kundi la wanamgambo la Hezbollah nchini Lebanon, linaloungwa mkono na Iran.

Chanzo: DPAE

Related Posts