Vifaa vya kisasa kutumika kuwanoa wanafunzi wa ukunga, uuguzi

Dar es Salaam. Wanafunzi kutoka vyuo 36 vinavyotoa elimu ya fani ya uuguzi na ukunga Tanzania Bara na Zanzibar watanufaika na vifaa vya kuwasaidia kusoma kwa vitendo ili kuwajengea umahiri wa utoaji huduma.

Vifaa hivyo ikiwamo midoli vitawasaidia kujifunza namna bora ya kumfanyia uchunguzi wa kina mjamzito na kumzalisha, pia kwa wasio wajawazito ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Vitendea kazi hivyo vya mafunzo vimetolewa kupitia mradi wa miaka mitano wa USAID wa afya ya mama na mtoto.

Katika awamu ya kwanza wanatarajia kutoa vifaa vyenye thamani ya Sh313.8 milioni kwa vyuo 10 kikiwamo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Akizungumza Dar es Salaam jana Agosti 28, 2024 wakati wa kukabidhi vifaa kwa Muhas, Ofisa Mshauri wa mradi huo, Alphonce Kalula amesema mkakati huo unatokana na changamoto walizobaini kuhusu hali ya upatikanaji wa mafunzo ya umahiri kwa wanafunzi wa sekta hiyo walio vyuoni.

“Tunataka kuwekeza kwa wanafunzi ili hata wakiajiriwa leo waweze kufanya kazi kwa kuwahudumua wajawazito hospitalini kwa sababu wanakuwa na uwezo ili kupunguza vifo vya mama na mtoto,” amesema.

Amesema mpango ni kuwafikia wanafunzi 200 kwa kila chuo kila mwaka, ambao watanufaika na matumizi ya vifaa hivyo.

“Tumeanza hapa Muhimbili tumewaletea vifaa vinavyofanana na uhalisia wa mazingira kama vya kumsaidia mama kujifungua na kufanya uchunguzi,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Redemptha Matindi amesema vifaa hivyo vitaleta ufanisi na hali ya kujiamini kwa kumuandaa mwanafunzi kwa utoaji huduma bora.

“Huduma ya afya inahitaji zaidi kumuandaa mwanafunzi kwa masomo ya vitendo, tumekuwa tukiona elimu ikitolewa na watu wanakuwa na ujuzi, imekuwa msaada mkubwa kwa mwanafunzi anapoingia kukutana na mgonjwa halisi akiwa ameshapata maarifa,” alisema.

Redemptha amesema dunia inakoelekea kuna mageuzi makubwa ya teknolojia na jamii inajitahidi kujua haki zake kwa kuwa inafikiwa na taarifa nyingi.

“Kuja na masomo kwa vitendo inatupunguzia malalamiko kutoka kwa wale wanaopokea huduma, lakini mwanafunzi anayekuwa amesoma ili aweze kupata cheti elimu ya vitendo na nadhari lazima ziende pamoja,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Uuguzi na Ukunga, Rozi Mgonja amesema wamepokea vifaa hivyo kwa furaha kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa.

“Vifaa hivi ni vizuri na imara, vitatusaidia kufundisha wanafunzi katika maabara ya masomo kwa vitendo na wakifaulu hapa wataenda kukutana na wagonjwa wodini.

“Ni jambo zuri linamfanya mwanafunzi asiende moja kwa moja kwa mgonjwa na kumfanya ajifunze mara nyingi ili akifika kwa mgonjwa aweze kumuhudumia kwa weledi zaidi,” amesema.

Amesema vifaa walivyopatiwa vinasaidia kumhudumia mjamzito kujifungua, uzazi wa mpango lakini kuwapima kina mama, akieleza vingine vitatumika kufanya uchunguzi.

Mwalimu na mkufunzi wa chuo hicho Maridhawa Jaji amesema vifaa hivyo wamepelekewa muda mwafaka kwa sababu wanahitaji zaidi kumfundisha mwanafunzi kwa vitendo.

Amesema midoli itawasaidia kumfundisha mwanafunzi namna bora ya kumzalisha mjamzito na kufanyia uchunguzi kwa vitendo.

Mwanafunzi wa mwaka watatu wa fani ya uuguzi na ukunga kutoka Muhas, Fridas Ally amesema vifaa hivyo vitawaongezea ujuzi wawapo darasani.

“Ni vifaa vinavyohusu zaidi masuala ya uzazi wa mpango na namna bora ya kujifungua, tunaahidi tutavitumia vizuri na kuleta tija inayotakiwa kwa kuwahudumia wagonjwa baada ya kumaliza masomo,” amesema.

Related Posts