Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo CPA Amoss Makala ametoa maelekezo kwa mkandarasi anayejenga jengo la ghorofa sita la Hospitali ya Mbagala mkoani Dar es Salaam kuhakikisha ifikapo Juni mwaka 2024 liwe limekamilika na kuanza kutoa huduma.
CPA Makala ametoa maelekezo hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Mbagala ikiwa ni sehemu ya ratiba ya kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Mbagala ya Wilaya kwani hatua ambayo imefikia ni nzuri lakini niwakumbushe hakikisheni hadi Juni mwakani hospitali hii iwe imekamilika na ukizingatia mwakani tunajambo letu,hivyo lazima hospitali ikamilike mambo yawe mazuri,”amesema CPA Makala.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika utagharimu Sh.bilioni na kwamba Chama Cha Mapinduzi kinamshukuru Rais DK.Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa kuridhia na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mbagara Rangi Tatu.
“Ujenzi wa hospitali hii wakati unaanza nikiwa Mkuu wa Dar es Salaam nilisimamia mchakato tangu ulipokuwa unaanza mpaka kumpata mkandarasi na sababu ni mahitaji makubwa ya huduma ya afya.Idadi ya watu Mbagala na Temeke ni kubwa.”
“Nawapongeza Meya na madiwani kwa kuhakikisha dhamira ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuleta huduma karibu na wananchi.Mmmeamua kujenga ghorofa na tunafahamu changamoto ya ya maeneo hivyo tuliamua kujenga ghorofa.
“Baada ya kuona kuna changamoto ya elimu katika mkoa wa Dar es Salaam tulipata fedha lakini shida ilikuwa maeneo, hivyo nilitoa maelekezo nikiwa Mkuu wa Mkoa huu tuanze kujengaSekondari za ghorofa na hata katika hospitali hii ujenzi wake ni wa ghorofa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbagala Abdallah Chaurembo amesema wanamshuru Raia Dk.Samia Suluhu Hassan kutoa fedha Sh.bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi huku wao pia wakitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu amemshukuru CPA Makala kwa kufanya ziara katika majimbo ya 10 ya Mkoa huo na ziara yake imekuwa na mafanikio makubwa.