Serikali yaanza uchunguzi chanzo ajali ya treni iliyojeruhi abiria 70

Kigoma. Serikali imesema imeanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali ya treni iliyosababisha watu 70 kujeruhiwa.

Awali, taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Jamila Mbarouk ilisema ajali hiyo ilitokea jana Jumatano Agosti 28, 2024 kati ya Stesheni ya Kazuramimba na Uvinza na watu 70 walijeruhiwa.

Treni hiyo ilikuwa imebeba abiria 571 kutokea mkoani Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Akizungumza leo Alhamisi Agosti 29, 2024 alipowatembelea na kuwajulia hali majeruhi wanne waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema uchunguzi huo umeanza tangu jana ukilenga kubaini chanzo cha ajali hiyo.

“Sisi kama TRC tumebeba dhamana kubwa ya watu kwa sababu ukiangalia kwenye ajali ya jana kulikuwa na abiria 571 na hadi ikifika Dar es Salaam inafika na abiria zaidi ya 1,000, unaweza kuona tuna dhamana ya watu wengi kiasi gani na siyo kwa treni moja karibia zote zinakuwa zimebeba watu wengi hadi treni ya mwendo kasi, ndiyo maana tunatakiwa kuwa makini kwenye usafiri wetu,”amesema Kadogosa.

Amesema mbali ya kuanza uchunguzi huo, lakini shirika linabeba dhamana ya kugharamia matibabu ya majeruhi wote wanaotibiwa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza ambao kwa sasa wamebaki sita na wale wanne walioko Hospitali

ya Maweni na shirika litahakikisha linagharamia usafiri wao baada ya matibabu.

Wakizungumzia maendeleo yao leo, majeruhi hao wamesema bado wanaendelea na matibabu hospitalini hapo, huku wengine wakisubiria majibu ya vipimo vya awali walivyochukuliwa.

Hamida Hamza amesema siku ya jana alikuwa na hali mbaya na maumivu makali sehemu za kifua, Mgongo na mbavu lakini majibu ya awali yameonesha hajavunjika isipokuwa ni maumivu ya ndani kwa ndani hivyo bado anaendelea kusubiria majibu ya vipimo vingine.

Naye, Kingoni Ndindigu amesema mkono wake umevunjika kwa ndani eneo la bega hivyo ameshaanza tiba na kwamba anatumaini atapona na kurudi kwenye majukumu yake ya kila siku.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Lameck Mdengo amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri na kupatiwa matibabu ya kibingwa na kwamba hakuna mgonjwa atakayepewa rufaa wajeruhi wote 4 watatibiwa hapo hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amesema Serikali itahakikisha inafuatilia kwa ukaribu maendeleo yao ili kuona wanapata matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani na kuendelea na maisha kama awali.

Related Posts