Musoma. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh30 milioni kama mchango wake kuchangia shughuli za Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 40 ya upadri wa Askofu Michael Msonganzila wa jimbo hilo.
Mchango huo umewasilishwa katika maadhimisho hayo leo Agosti 29, 2024 mjini Musoma na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Rais Samia.
Ndejembi amesema Serikali inatambua mchango wa viongozi wa dini katika kukuza na kuhimiza amani, umoja na upendo miongoni mwa Watanzania.
“Rais Samia amesema Serikali inatambua mchango wenu viongozi wa dini na itaendelea kushirikiana na ninyi ili kufikia malengo ya wananchi wetu ya kuwa na maendeleo endelevu,” amesema.
Amesema Serikali pamoja na mambo mengine inatambua kuwa mchango wa viongozi hao wa dini utasaidia katika kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu 2025.
Amesema kutokana na hali hiyo, amewaomba viongozi hao kuendelea kuhubiri amani na upendo miongoni mwa Watanzania ili chaguzi hizo ziweze kufanyika kama ilivyopangwa kwa maslahi ya ustawi wa nchi.
Ndejembi amempongeza Askofu Msonganzila kwa kufikisha miaka 40 ya upadri huku akisema miaka hiyo ni mingi na kwamba askofu huyo ametumia miaka hiyo vema katika kulitumikia kanisa na jamii nzima.
“Miaka 40 ni rahisi na michache sana kwa kuitamka lakini ukiiweka kwenye vitendo ni muda mrefu sana, mfano mimi hapa nina miaka 41, ina maana askofu ameanza kuwa padri nikiwa na mwaka mmoja ni muda mrefu na unastahili pongezi. Hii ina maana askofu ametumia muda mwingi sana kuwatumia wananchi kiimani na kijamii, tuendelee kumwombea apate miaka mingine 40,” amesema Ndejembi.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Askofu Msonganzila amesema lengo la kufanya Jubilei hiyo, ni kutaka kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomuwezesha kufikia hapo alipo kuanzia kuzaliwa, upadrisho na uaskofu.
Amewataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuondokana na changamoto za magonjwa hasa yasiyo ya kuambukizwa ambayo yanaweza kutibiwa endapo yatagundulika mapema.
“Mimi hapa kabla ya maadhimisho haya ilinibidi niende Hospitali ya Bugando, nikaonana na wataalamu ambao baada ya kunipima walisema niko vizuri na kuniruhusu kuendelea na shughuli hii,” amesema.
Amesema Watanzania wengi wana utaratibu wa kwenda hospitalini pale wanapojisikia wanaumwa, jambo ambalo sio jema na kwamba kutokana na ongezeko la magonjwa ni vema wakawa na utaratibu wa kwenda hospitalini kupima mara kwa mara kwani wana wajibu na haki ya kutunza afya zao.
“Mimi leo niko hapa kubwa zaidi ni kutaka kusema asante kwa Mungu wangu pia niwakumbushe Watanzania tujenge utamaduni wa kujua afya zetu, wenye bima tumieni bima zenu mbali na kwa ajili ya matibabu lakini kujua hali zenu za kiafya,” ameongeza Askofu Msonganzila.
Ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Rais kwa mchango wake alioutoa kwa ajili ya kuchangia shughuli za kanisa, huku akiahidi kuendelea kumuombea ili Mungu ampe hekima zaidi katika kuwaongoza Watanzania.
Akitoa pongezi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema baraza hilo linaona fahari kutokana na kazi ambazo Askofu Msonganzila anazozifanya kwa kanisa na jamii kwa ujumla.
Amesema katika miaka yake 40 ya upadri ikiwemo miaka 17 ya uaskofu, Askofu Msonganzila amekuwa kielelezo na kinara wa ustawi wa jamii kiimani, kimwili na kisaikolojia.
“Umefanya mambo mengi ikiwemo kuwa kimbilio la mabinti walioathirika na ukatili wa kijinsia umejenga makazi kwa mabinti hao na kuwapa fursa ya wao kusikika na wengine kuweza kufikia malengo yao,” amesema Askofu Kasala.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Matthew amempongeza askofu huyo kwa kutimiza miaka 40 ya upadri huku akimuomba kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kutawaliwa na amani na umoja.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, maaskofu na mapadri kutoka majimbo mbalimbali pamoja Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Kadinali Polycap Pengo.