Maofisa ustawi wa jamii waonywa kupoteza ushahidi kwa rushwa

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kinondoni mkoani hapa imewaonya maofisa ustawi wa jamii kujiepusha na tabia ya kula rushwa ili wapoteze ushahidi katika malalamiko ya wananchi yanayotakiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Hayo yamesemwa leo Agosti 29, 2024 na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni kwa mfumo wa taasisi hiyo, Christian Nyakizee wakati wa mafunzo na maofisa hao, akisema kwa mwaka 2023/24 wamepokea mashauri 41 ya ukatili wa kingono ambayo 37 yaliwahusu watoto na manne yakiwa ya watu wazima.

“Kutokana na takwimu hizi kundi kubwa linaloathirika na ukatili wa kingono ni watoto na hivi karibuni jamii yetu imekuwa  na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu ukatili kwa kijinsia na kingono na kuibua hisia huku rushwa ikiwa ni tatizo,” amesema Nyakizee.

Amesema kumekuwa na malalamiko mengi yanayochangia vitendo vya ukatili kuongezeka, ambapo waathirika wamekuwa wakiona aibu kufikisha taarifa zao kwenye vyombo vya sheria na ustawi wa jamii, kwani huwa hayachukuliwi kwa uzito.

Nyakizee amesema kumekuwa na tabia ya wahusika kutotimiza wajibu wao na kutoa rushwa ili mashauri yao yasipelekwe mbele au kutolewa ushahidi unaohitajika kwenye vyombo vya usimamizi wa sheria. 

“Kuendelea kwa mambo hayo yamekuwa yakichangia kuwaathiriri wahusika kisaikolojia na kimwili na hali hiyo imefanya wananchi kufikiri Serikali haitimizi wajibu wake kupitia watu wa ustawi wa jamii kwa wananchi,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kinondoni, Mwanasheria Manispaa hiyo, Leah Mnzava amesema migogoro mingi inaanzia kwenye Serikali za mitaa na mara nyingi haifiki mwisho.

“Elimu hii inayotolewa hapa ifike huko hasa kwa wale wajumbe ambao wanakaa karibu na wanaofanya hivi vitendo kwani ni ukiukwaji wa haki za binadamu,” amesema Mnzava.

Amesema maofisa ustawi wa jamii wanatakiwa kutimiza wajibu wao kwani wanaweza kufanyakazi vizuri lakini wakajitia doa kwa kitu kidogo na kushindwa kumaliza kesi iliyopo mbele yao.

Ofisa Ustawi wa Jamii, Manispaa ya Kinondoni, Neema Mwalubilo amesema changamoto inayowakabili ni familia kutotaka kuendelezwa kwa kesi hivyo wanahangaika kupita njia mbalimbali ikiwepo utoaji wa rushwa.

“Familia zimekuwa ni shida utakuta mtu amefanya tukio hivyo familia nzima wanaungana naye kwa kutoa rushwa ili shauri lisifike sehemu husika kwa kuhofia kuwa ndugu yao atafungwa miaka mingi,” amesema Neema.

Related Posts