Dar es Salaam. Wadau takribani 15 wa sekta ya hoteli nchini wametakiwa kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa kutambua viashiria na kutoa taarifa kwenye mamlaka za Serikali.
Hayo yameelezwa Agosti 29, 2024 Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mtandao wa Taifa Wakupambana na Usafirishaji haramu wa binadamu Tanzania, Edwin Mugambila katika ufunguzi wa mafunzo yaliyofadhiliwa na Ubalozi wa Marekani nchini.
Amesema Tanzania imeendelea kuwa lango na mapitio ya usafirishaji haramu wa binadamu hasa katika hoteli, hivyo kuna haja ya kutoa mafunzo kwa watumishi ili kudhibiti janga hilo.
Amesema miongoni mwa makosa hayo ni kuwatumikisha watoto kingono katika hoteli hizo.
“Napenda kuwakumbusha kuwa nchi ina sheria kali, vitendo vyenye viashiria vya kingono na mtoto ndani ya hotel inaadhabu isiyopungua miaka 30 au maisha jela, au kulipa faini inayofikia Sh50 milioni mpaka Sh300 milioni na kufilisi hoteli kwa kutaifisha mali zote za hoteli hiyo,” amesema.
Naibu Kamishna wa Sekeretarieti ya Kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ahmad Mwendadi amesema wameandaa mikakati ya kutosha kuhakikisha wanapambana na usafirishaji huo haramu wa binadamu ambao ni uhalifu kama uhalilifu wowote.
“Sektarieti hii inaratibu taasisis zisizo za kiserikali katika masuala ya usafirishaji haramu wa binadamu, ikishirikiana na Jeshi la Polisi na Idara vya Uhamiaji, hasa katika upelelezi kwa wasio raia wa Tanzania na wale raia Watanzania wanaowasafirisha kwenda nje ya nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa, kwa Watanzania waliopo nje ya nchi balozi za Tanzania zilizopo katika nchi hizo zimekuwa zikiwarejesha wale waliosafirishwa kwa njia haramu.
Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Michael Battle amesema asilimia 50 ya misaada wanayoitoa kila mwaka imelenga kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu ambao umewaathiri zaidi wanawake na watoto.
“Marekani kwa sasa imeelekeza nguvu kubwa kuhakikisha inatokomeza mtandao mbaya wa usafirishaji haramu wa binadamu dunia kote,” amesema.
Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kutokomeza uhalifu huo tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwaka 2023.