Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imetupilia mbali shauri lililofunguliwa na wakili Leonard Mashabara la kuitaka ifanye marejeo ya kesi ya jinai inayowakabili washtakiwa wanne wanaodaiwa kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile, binti wa Yombo Dovya, Dar es Salaam kutokana na kuwapo dosari kisheria.
Dosari hizo ni kuwaingiza kwenye shauri hilo watu wasiohusika kwenye kesi ya msingi.
Katika shauri hilo, Mashabara aliiomba Mahakama kupitia uhalali wa uwakilishi wa washtakiwa katika kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024, inayowakabili askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu kama Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Shauri hilo lililowasilishwa mahakamani hapo Agosti 23, 2024 mbele ya Jaji Suleiman Hassan, wajibu maombi walikuwa ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), washtakiwa hao wanne pamoja na mawakili wanaowawakilisha ambao pia ni wanne.
Akitoa uamuzi leo Alhamisi Agosti 29, 2024 Jaji Hassan amesema mmoja wa wajibu maombi ambaye anawatetea mawakili wanaowawakilisha kina Nyundo, aliwasilisha pingamizi akiwa na hoja sita kuhusu uhalali wa kufunguliwa shauri hilo.
Hata hivyo, amesema hoja mbili ziliondolewa na kubaki nne ambazo ziliwasilishwa mbele ya Mahakama Kuu na kuungwa mkono na wajibu maombi wengine.
Jaji amesema kati ya hoja hizo nne, ni moja pekee iliyodai baadhi ya wajibu maombi hawahusiki kwenye kesi ya msingi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ndiyo iliyokubaliwa.
Amewataja wajibu maombi hao kuwa ni TLS, AG na mawakili wanaowatetea Nyundo na wenzake.
Amesema wajibu maombi hao hawawezi kujibu maombi kwenye shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu kwa sababu hawahusiki na kesi ya msingi iliyoko kwenye Mahakama ya chini.
“Hivyo katika shauri hili mleta maombi (Mashabara), alishirikisha watu ambao si sehemu ya kesi ya msingi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria… Hivyo, uamuzi wa Mahakama ni kwamba maombi hayo hayako sawa kisheria na Mahakama inayatupilia mbali,” amesema Jaji Hassan.
Katika shauri hilo wajibu maombi walikuwa 11, wa kwanza hadi wa saba waliwakilishwa na wanasheria wao, huku wa nane hadi wa 11 ambao ni washtakiwa katika kesi ya kubaka kwa kikundi hawakuwa na wakili.
Akizungumza nje ya Mahakama, wakili Robert Owino akiwawakilisha mawakili wenzake ambao wote wanawawakilisha kina Nyundo, amesema baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali maombi hayo, kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa, iwapo mleta maombi hatakata rufaa kuhusu uamuzi uliotolewa.
Kwa upande wake, wakili Emmanuel Anthony anayemwakilisha Mashabara amesema wakati wanafungua shauri hilo waliwajumuisha watu wengine ambao walidhani walikuwa ni mahususi kusikilizwa, lakini Mahakama Kuu imeona kuwa watu wale hawakupaswa kuwapo kwenye shauri hilo.
Amesema kwa msingi huo, shauri walilofungua limeondolewa na wameupokea uamuzi huo ambao hauathiri uamuzi wa mteja wake.
“Kwa hiyo maelekezo aliyonayo (Mashabara) ni kwamba nikarekebishe yale maombi na tuyarudishe mahakamani, kitu ambacho tumeshakifanya, kwa hiyo tunategemea kuanzia labda kesho tunaweza kuwa na majibu ya nini tutakachofanya kutokana na hayo maombi yetu hapahapa Mahakama Kuu,” amesema Anthony.
Kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 dhidi ya kina Nyundo imepangwa kutajwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kesho Agosti 30, 2024.
Ilianza kusikilizwa Agosti 20 kwa siku nne mfululizo hadi Agosti 23 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule. Tayari mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi.