MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara timu ya Yanga wameanza vyema kampeni za kutetea ubingwa wa michuano hiyo kwa msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, lakini kocha wa timu hiyo ya Wananchi, Miguel Gamondi amelalamikia nafasi nyingi wanazopoteza nyota wake.
“Kipindi cha kwanza tumetengeneza nafasi saba au nane, lakini tumeitumia moja na hili ndio tatizo letu,” alisema Gamondi na kuongeza: “Tunatakiwa kuwa bora zaidi katika hilo. Hata hivyo, tunashukuru kwa kupata pointi tatu.”
Kocha wa Kagera Sugar, Paul Nkata alisifu ubora wa wapinzani wao akisema unapokutana na timu ambayo wachezaji wake 14 wameitwa kwenye timu za taifa, sio jambo rahisi kucheza dhidi yao.
Umahiri wa kipa wa Kagera, Ramadhan Chalamanda aliokoa hatari nyingi kiushujaa, huku nyota wa Yanga kama Prince Dube, Pacome Zouzoua, Aziz Ki walikosa utulivu mbele ya lango na kupoteza nafasi nyingi zilizoonekana ni nyepesi kufunga kwa wachezaji wa kiwango chao.
Maxi Nzengeli aliifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 26 akifanya juhudi binafsi na kupiga shuti la nje ya boksi akitumia asisti ya Pacome, kabla ya mtokea benchini aliye katika kiwango bora sana Clement Mzize kufunga la pili dakika za jiooni akimalizia pasi ya Aziz Ki.
Nyota wa Yanga, Prince Dube, licha ya kuonyesha makali yake akiwa na kikosi hicho katika mashindano mbalimbali, ila hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza alikosa utulivu wa kutumia vyema nafasi za wazi alizotengenezewa na nyota wenzake.
Katika kipindi cha kwanza, Yanga ilipiga mashuti sita yaliyolenga lango (shot on target) dhidi ya moja tu la wenyeji, huku Prince Dube pekee akikosa nafasi tatu za wazi za kufunga ikiwemo dakika ya pili ya mchezo, dakika ya 19 na 21, alipotengenezewa na Pacome.
Mbali na Dube ila hata Stephane Aziz KI alishindwa kutumia vyema nafasi ya wazi aliyoipata dakika ya nane huku shujaa wa Kagera Sugar akiwa ni kipa, Ramadhan Chalamanda aliyeokoa michomo mingi kabla ya kuruhusu bao la Maxi Mpia Nzengeli.
BAO LAIAMSHA KAGERA SUGAR
Wenyeji Kagera ilianza mchezo taratibu na kucheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda hadi iliporuhusu bao la kwanza na kuanza kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza huku ikimtegemea zaidi mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Deogratis Mafie.
Mbali na kushambulia kwa tahadhari Kagera ila iliwategemea zaidi viungo, Joseph Mahundi na Nassoro Kapama ambao walianza kuonekana kipindi cha pili cha mchezo huo tofauti na cha kwanza ambacho kwa kiasi kikubwa walizidiwa na ubora wa viungo wa Yanga.
Yanga imeendeleza rekodi yake nzuri kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Kagera Sugar mabao 3-0, Januari 15, 2020, wakati huo ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Luc Eymael, haijawahi tena kupoteza hadi leo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Tangu mwaka 2020, Yanga imekutana na Kagera Sugar katika jumla ya michezo 10, ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo imeshinda minane na kutoka sare miwili tu huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 18 na kuruhusu kutikiswa mara tatu.
Pia, Yanga imeendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Ihefu ambayo inajulikana kama Singida Black Stars mabao 2-1, Oktoba 4, 2023, haijapoteza tena hadi sasa.
Mchezo wa mwisho kwa Yanga kupoteza wa mashindano ulikuwa ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilipochapwa kwa penalti 3-2, baada ya suluhu michezo yote miwili Aprili 5, mwaka huu.
Baada ya mchezo huo, Yanga imecheza jumla ya michezo 19 ya mashindano tofauti ambapo kati ya hiyo imeshinda 18 na kutoka suluhu mmoja tu uliokuwa dhidi ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Aprili 24, 2024.
Wakati Yanga ikiwa ndio kwanza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kwa upande wa wenyeji wao Kagera Sugar huu unakuwa ni wa pili chini ya kocha mpya raia wa Uganda, Nkata huku ikishindwa kupata ushindi wowote hadi sasa.
Kagera ilifungua pazia la Ligi Kuu Bara Agosti 24, mwaka huu kwenye Uwanja wake wa Kaitaba ambapo iliambulia pia kipigo cha bao 1-0, dhidi ya Singida Black Stars lililofungwa na beki wa timu hiyo, Anthony Tra Bi Tra dakika ya 90 ya mchezo.
YANGA KUKUMBANA NA ADHABU
Yanga itakutana na adhabu kutoka Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kosa la kutojumuisha mchezaji yeyote wa timu za vijana katika kikosi cha jana.
Kanuni ya 17:6 kipengele cha tatu kuhusu taratibu za mchezo inaeleza kwamba, “Klabu ya Ligi Kuu inawajibika kujumuisha wachezaji wasiopungua wawili kutoka katika timu zake za vijana kwenye orodha ya wachezaji 21 kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara.”
Wachezaji walioanzia benchini ni Aboutwalib Mshery, Aziz Andambwile, Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Shekhan Ibrahim, Duke Abuya, Clatous Chama, Kennedy Musonda na Clement Mzize, hivyo kuonyesha wazi Yanga imeivunja kanuni hiyo mpya msimu huu.
Kikosi cha Kagera Sugar kilichoanza ni Ramadhan Chalamanda, Joseph Mahundi, Emmanuel Charles, Nassoro Kapama, Chilo Mkama, Salehe Seif, Jofrey Manyasi, Peter Lwasa, Deogratius Mafie, Hijja Shamte, Datius Peter.
Kikosi cha Yanga kilichoanza ni Djigui Diarra, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Khalid Aucho, Maxi Mpia Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua.