KMC yabanwa mbavu nyumbani na Coastal, Matampi akirihusu bao

KINARA wa Clean Sheet kwa msimu uliopita, Ley Matampi wa Coastala Union ameuamza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kwa kutunguliwa wakati timu hiyo ikitoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya KMC.

Matampi aliyemaliza msimu uliopita na Clean Sheet 19 na kutwaa tuzo ya Kipa Bora wa msimu huo, alitunguliwa kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar es Salaam na kuiofanya timu hiyo kuvuna pointi moja ugenini.

Katika mechi mbili za mwisho za mssimu uliopita, kipa huyo raia wa DR Congo hakuruhusu mabao na kumpiku Diarra Djigui wa Yanga aliyemaliza na Clean Sheet 18, japo hakucheza mechi ya mwisho wakati wa kufunga msimu huo.

Kipa huyo aliyeanza kuonekana kwenye mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati Coastal ikilazimishwa suluhu na AS Bravos ya Angola na kung’olewa raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 3-0, katika mechi ya jana alionyesha umahiri wake, kabla ya kutunguliwa na Ibrahim Elias dakika ya 32 iliyowatanguliza wenyeji.

Hata hivyo kipindi cha pili Wagosi walipambana na dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho ya pambano hilo, ilichomoa bao hilo kwa mkwaju wa penalti.

Penalti hiyo  ilipigwa na Maabad Maulid baada ya  kipa wa KMC, Fabien Mutombora kumsuka mchezaji wa Coastal na mwamuzi kuamuru mkwaju huo uliowaokoa Wagosi wasipoteze mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa kila timu.

Kwa ujumla mchezo huo ulikuwa na ushindani wa hali ya juu ukizingatia kwamba timu zote zilikuwa zikishuka dimbani kwa mara ya kwanza msimu huu huku wenyeji KMC wakipania kutoweka rekodi mbaya ya kupoteza mechi uwanja wa nyumbani wanaoutumia kwa msimu huu.

Katika kutafuta ushindi, timu hizo zilishambuliana kwa zamu, huku matumizi makubwa ya nguvu na kasi vikitawala kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Licha ya Coastal kuruhusu bao kipindi cha kwanza, haikuwa sababu ya wachezaji wa timu hiyo kuacha kupambana hadi walipofanikisha kusawazisha na kuambulia pointi moja.

Sare hiyo imekuwa ni muendelezo wa mechi tatu mfululizo za ligi kwa timu hizo kushindwa kupatikana mbabe kwani msimu uliopita mechi zote mbili za ligi matokeo yalikuwa 0-0.

Rekodi za jumla zinaonyesha kwamba, hiyo ni sare ya nane katika mechi 13 walizokutana wawili hao ndani ya Ligi Kuu Bara tangu 2018/19 ambao KMC ilipanda daraja. Katika mechi hizo, KMC imeshinda mbili na Coastal ikishinda tatu.

KMC: Fabien Mutombora, Ken Ally, Juma Ramadhan, Ibrahim Elias, Rashid Chambo, Ali Shabani, Pascal Mussa, Fredy Tangalo, Redemtus Mussa, Abdallah Said na Shomary Rahim.

COASTAL: Ley Matambi, Jackson Shiga, Abdallah Hassan, Greyson Gwalala, Amagu Anguti, Mbaraka Yusuf, Hernest Malonga, Mukrim Issa, Mirajy Abdallah, Kalumba Banza na Semfuko Charles.

Related Posts