TUANZE kuwaandaa warithi wa nyota wetu wawili wa timu ya taifa, Taifa Stars, nahodha Mbwana Samatta na msaidizi wake Saimon Msuva.
Hawa ni wachezaji wawili ambao wamejitoa na kuipambania jezi ya Stars kwa muda mrefu na kwa uzalendo wa hali ya juu katika nyakati za shida na raha na hilo linathibitishwa na takwimu zao za kufumania nyavu.
Ukiondoa Mrisho Ngassa ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Stars akiwa na mabao 25, Samatta na Msuva ndio wanaofuatia kwa kupachika idadi kubwa ya mabao katika kikosi cha timu hiyo.
Wawili hao wamefunga idadi sawa ya mabao ambayo ni 22 huku anayewafuatia akiwa ni John Bocco ambaye tayari ameshatundika daruga katika timu ya taifa akiwa amefumania nyavu mara 16.
Haiishii katika kufunga mabao tu bali pia Msuva na Samatta ni miongoni mwa wachezaji waliocheza idadi kubwa ya mechi katika kikosi cha Stars na hilo ni uthibitisho wa umuhimu wao.
Msuva anashika nafasi ya nne kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za Stars akiwa ameingia uwanjani katika michezo 92 wakati huo Samatta akiwa anashika nafasi ya nane katika chati hiyo akiwa amecheza idadi ya michezo 79.
Lakini lazima tufahamu kwamba wawili hao wanaelekea ukingoni hivi sasa kwa maana ya kiwango na hata umri hivyo muda sio mrefu ujao wanaweza kuweka viatu ukutani na kuamua kupumzika kuitumikia Stars.
Sasa kabla hawajaamua kufanya hivyo inabidi tufanye kazi ya ziada ya kusaka watu ambao wataendeleza pale ambako wawili hao wataishia katika kuiwakilisha kwao Stars badala ya kujisahau na kuona kama watacheza kila siku.
Nyakati hazitawasubiria Samatta na Msuva na hilo liko wazi hivyo muda utakapofika wa wao kuiaga Stars, kunatakiwa kuwepo tayari vijana wa kuwapokea vijiti na sio ndio kuanza kutafuta jambo ambalo litasababisha presha kwa vijana.