Dabo aingiwa ubaridi Azam | Mwanaspoti

KOCHA mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema anajua kila kinachoendelea kwa sasa juu ya hatma yake klabuni hapo, lakini hana hofu na kutemeshwa kibarua kutokana na matokeo mabaya iliyopata timu hiyo hivi karibuni na hasa baada ya kuondoshwa katika hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kauli ya Dabo inajiri baada ya juzi timu hiyo kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania katika mchezo mkali na wa kusisimua wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa timu hizo msimu huu uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tangu ing’olewa CAF na APR ya Rwanda.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Senegal, alisema, kabla ya kuja Azam alikuwa timu nyingine, hivyo hana hofu na kitakachotokea juu yake, huku akiweka wazi bado anaamini ana wachezaji wazuri wa kufanya makubwa ingawa wanahitaji muda zaidi kwani kikosi ni kipya kabisa.

“Kila kitu kilibadilika kwetu baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kutolewa kwa sababu sote tulihuzunishwa na kilichotokea, ingawa hatuwezi kuangalia nyuma na badala yake tunawekeza nguvu katika mashindano ya ndani,” alisema Dabo aliyeiwezesha Azam msimu uliopita kumaliza ya pili katika Ligi Kuu na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa tangu ilipoishiriki mara ya mwisho mwaka 2015.

Dabo alisema wachezaji wengi katika kikosi hicho ni wapya na wanahitaji muda wa kuzoeana hivyo sio suala la siku moja au mbili kutengeneza muunganiko wa kiuchezaji kwa kila mmoja wao, ingawa kuna maendeleo mazuri kwa baadhi yao kikosini.

“Nilikuwa timu nyingine kabla ya kuwepo Azam, naweza nikabakia hapa kwa msimu huu hadi mwisho au vinginevyo, kwangu ni changamoto ambayo nakabiliana nayo ili kutengeneza kikosi imara chenye ushindani katika mashindano ya ndani kwa sasa,” alisema Dabo.

Azam imeanza vibaya msimu huu kwani msimu uliopita ilipata pointi zote sita mbele ya JKT Tanzania baada ya kushinda nyumbani mabao 2-1, Desemba 11, 2023, kisha kuibuka tena kidedea na ushindi wa mabao 2-0, mechi iliyopigwa Mei 21, 2024.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kushindwa kupata mbabe katika Ligi Kuu Bara ilikuwa Oktoba 30, 2020, zilipofungana bao 1-1, ambapo JKT ilifunga bao kupitia kwa Michael Aidan katika dakika ya 43, kisha Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ kusawazisha dakika ya  78.

Azam iliingia katika mchezo huo na JKT baada ya kuondolewa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1, dhidi ya APR ya Rwanda, kufuatia kuanza vyema nyumbani kwa ushindi wa bao 1-0, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

Msimu huu pekee Azam imeshiriki michuano mitatu tofauti ikianza na Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara na katika mashindano hayo timu hiyo imecheza michezo mitano ambapo kati ya hiyo imefunga mabao saba huku ikiruhusu manane. Katika Ngao ilipoteza fainali mbele ya Yanga kwa 4-1.

Related Posts