Dar es Salaam. Ukiihesabu miaka minne kwa umri wa binadamu, basi ni mtoto anayemudu kutembea, anakimbia na sasa anatamka karibu kila neno.
Hicho ndicho kipindi ambacho Bakari Machumu amehudumu nafasi ya mkurugenzi mtendaji katika miaka yake 20 aliyofanya kazi kwenye Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Machumu amekuwa kwenye nafasi hiyo ya juu tangu Aprili 29, mwaka 2021 alipotangazwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Stephen Gitagama hadi sasa Agosti 31, 2024 anapostaafu.
Ingawa ameng’atuka mapema katika nafasi hiyo ya juu, Machumu anajivunia mafanikio yanayoifanya kampuni hiyo itazamwe na jamii kwa jicho la matumaini, ikiakisi kaulimbiu yake ‘Tunaliwezesha Taifa’.
Katika mahojiano maalumu aliyofanya na gazeti hili, Machumu anasema wakati anaondoka, inapaswa kueleweka kuwa, ukuaji wa MCL katika miaka ijayo utategemea kuendelezwa kwa misingi yake ambayo ni ubunifu na kuzingatia maboresho.
“Kwa hiyo ninaondoka MCL nikiwa ninaiangalia kwa ukubwa huo na nikijivunia kuwa sehemu ya safari hiyo. Naiona ikiendelea kufanya hivyo kama itabaki katika misingi ileile na ina fursa ya kukua,” anaeleza.
Anasema anaondoka MCL, ikiwa moja ya kampuni kubwa, yenye nguvu na inayofuatiliwa na makundi mbalimbali kutokana na uwezo wake wa kuleta matokeo kwenye jamii.
Kwa kadri jamii inavyoifuatilia MCL, anasema ndivyo watendaji wake wanavyopaswa kuwajibika kuhakikisha hawawaangushi wanaoifuatilia.
“Tunatakiwa tuheshimu kwamba watu wanaiangalia MCL kwa sura tofauti. Ninaposema watu, nazungumzia jamii zote, yaani Serikali, sekta binafsi na wananchi wote wanaingalia Mwananchi kwa jicho la matumaini, tusiwaangushe.” “Nguvu iliyonayo MCL haipaswi kutupanda vichwani tukaitumia vibaya. Ni nguvu inayotakiwa kutumika vizuri kuchochea maendeleo ya nchi hii na mtu mmojammoja,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Machumu, msingi wa chochote kinachofanywa katika kampuni hiyo ni kuliwezesha Taifa, ama kwa kuibua udhaifu ili urekebishwe na kuokoa maisha ya watu au kuonyesha fursa jamii izichangamkie.
“Hiyo ndiyo nguvu tuliyonayo na sio nguvu ya kwenda mbele unasema mimi ni MCL nitakushughulikia, hapana. Hiyo utashughulikiwa wewe,” anaeleza.
Ingawa mitihani ni sehemu ya maisha katika uongozi, Machumu anasema uamuzi uliohusisha kuwasimamisha kazi wahariri wanne katika chumba cha habari, ndiyo uliokuwa mtihani mgumu zaidi kwake.
Mtihani huo anasema ulikuwa mgumu kwa sababu alitakiwa kufanya uamuzi huo, wakati ambao hakuwa na ushahidi uliojitosheleza wa tuhuma dhidi ya wahariri hao.
“Pale nilijitafuta nikasema hawa ni watu wanaoripoti kwangu, wametuhumiwa walivyotuhumiwa, sijapewa ushahidi wa kutosha, lakini natakiwa nitekeleze, nikitekeleza maana yake nini.”
“Je, mimi nimesimama na watu ninaowaongoza au nimewatosa ninaowaongoza, nitalala usingizi kwa mtindo huo? Moyo wangu ukawa unakataa,” anaeleza.
Hata hivyo, anaeleza umahiri wa uongozi wa NMG unaotoa nafasi kwa viongozi kujadiliana kuhusu masuala yanayolinda uhai wa kampuni na wafanyakazi wake, ndiyo uliomwezesha kuuvuka mtihani huo.
Anaeleza mazungumzo yalifanyika na walikubaliana kuwasimamisha na si kuwafukuza kazi, kisha kujiridhisha kwa kufanya uchunguzi wa kina na baadaye walibaini wahariri hao hawakuwa na hatia.
“Tuliwarudisha kwa gharama kubwa zaidi kwa sababu nafasi zao tulishaweka watu wengine, bodi ililazimika kutengeneza nafasi nyingine nne kwenye bajeti yake ili kuwapa nafasi ya kuendelea kuwepo. Kwa sababu kulikuwa na ngao hiyo, ndiyo sababu niliahirisha kujiuzulu, lakini isingekuwepo kile kilikuwa kipindi cha mimi kubwaga manyanga na nikasema ngoja nikalime,” anasema.
Nafasi yake ya ukurugenzi wa MCL, anasema mara kadhaa imewahi kumtofautisha kimtazamo na viongozi mbalimbali ndani ya Serikali, hasa kutokana na baadhi ya maudhui yanazochapishwa na magazeti ya kampuni ya Mwananchi.
“Hiyo haiepukiki, lakini tumetokaje hapo? Mimi nimekuwa nikitumia sana kueleza kwamba hakuna chochote tutakachofaidika nacho kwa kuishutumu Serikali au kiongozi yeyote.
“Hata Aga Khan aliwahi kusema hakuanzisha vyombo vya habari, viwe sauti ya wapinzani, chama kilichopo madarakani au mtu yeyote asiyeenda sawa na jamii, bali ameanzisha ili visaidie kuleta matokeo chanya kwenye jamii tunayoishi,” anaeleza.
Ikitokea kutofautiana kwa mitazamo, Machumu anasema aghalabu hujikita kueleza nini dhima ya MCL, sera ya chumba cha habari na kama kuna makosa ni ya kibinadamu.
“Lakini haijawahi kuwa sera ya MCL kwamba kusimama kumshughulikia mtu fulani. Bodi hairuhusu, sera zetu haziruhusu na ndiyo sababu bodi ileile inayokulinda kufanya uandishi wa habari kwa uhuru, ni hiyohiyo inayokushughulikia ukiikanyaga sera yake,” anaeleza.
Mahojiano na wakuu wa nchi
Machumu ambaye amefanya mahojiano mara kadhaa na wakuu wa nchi, anasema hadi mkuu wa nchi anakubali kufanya mahojiano na mwandishi, inatokana na kushawishika na jambo fulani, ikiwemo nia njema ya mwandishi.
“Kwa hiyo anakuona kabisa si tishio kwake au haulengi kwenda kumuaibisha unapomfanyia mahojiano. Nadhani tatizo tunalolitengeneza ni kwamba unakuja kutaka taarifa kutoka kwangu, alafu unanichafua au kunivuruga ukitarajia nitakupa taarifa, sitakupa,” anaeleza.
Siri pekee ya kufanikiwa kupata mahojiano na watu wenye hadhi hiyo, anasema ni kuwafanya waamini unahitaji taarifa kutoka kwao, kuwa mnyenyekevu, mwadilifu na mwenye heshima.
“Ikijengeka tabia kwamba wewe ndivyo ulivyo na ukifanikiwa kufanya mahojiano na mmoja, mwingine akiona, atakuwa sawa kufanya mahojiano na wewe,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema mara nyingi amekuwa akifanya hivyo mwenyewe, kuonyesha kuwa, licha ya ukurugenzi wake bado ni mwanahabari.
“Tulifanya mahojiano na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipokuwa mgombea wa nafasi ya urais, aliyekuwa kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, hayati Maalum Seif Sharif Hamad, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Job Ndugai akiwa Spika wa Bunge na Rais Samia Suluhu Hassan mara mbili,” anaeleza.
Alipoulizwa kuhusu msingi wa kuanzishwa kwa Jukwaa la Rising Woman, Machumu anasema ilitokana na sehemu ya malengo ya MCL kutafuta mbinu za kuzalisha katika nyakati ambazo magazeti si biashara kubwa kama ilivyokuwa zamani.
“Mitandao ya kijamii iliharibu soko, kwa hiyo kukawa na msukosuko. Kwenye msukosuko huo tukawa tunajitafuta tunafanya nini ili tuvuke. Ujio wa Rising Woman ulilenga kufanya uandishi wa habari wa matukio eneo ambalo halikuwa linatazamwa zaidi,” anasema.
Katikati ya mazingira hayo, anaeleza viongozi wenzake walimshauri juu ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo, huku wakiwa na wasiwasi wa kupingwa, kwa kuwa MCL yenyewe haijafikia usawa wa asilimia 50 kwa 50 katika uongozi.
Anaeleza jukwaa hilo liliwavutia wengi hadi kufikia hatua ya kupata ushiriki wa Rais Samia.
Machumu anasema mwaka huu MCL ilifikia uwiano wa 40 kwa 60 katika uongozi, ingawa kwa sasa baadhi yao wamepata fursa katika maeneo mengine na wamekwenda huko, hivyo kwa kiasi fulani uwiano huo umerudi nyuma. Kurudi nyuma huko, anasema kunatokana na uchache wa wanawake wenye sifa zinazohitajika, hivyo kampuni nyingi zinawagombea.
Kwa mujibu wa Machumu, safari yake ya kuingia MCL ilianza kwa kushawishiwa kuomba nafasi na wafanyakazi wenzake aliokuwa anafanya kazi nao awali.
Hata hivyo, anasema alipofuatilia nafasi hiyo ya maombi, alikuta muda umeshapita, lakini baadaye ilitangazwa tena na akajaribu kuomba.
“Wakati nimepata ile nafasi, mama yangu aliniuliza Bakari wewe unaondoka ulipo ukiwa mhariri wa habari, unakokwenda unaenda kuwa mhariri wa biashara, mbona unarudi nyuma? Nilimwambia mama ile ni kampuni yenye hadhi ya kimataifa, nitajifunza zaidi na nitapata uzoefu zaidi na mshahara mnono,” anasema.
Anaeleza aliingia MCL akiwa na mtazamo wa ukubwa wake kutokana na historia ya ukubwa wa NMG.
Gazeti nyakati za uchaguzi
Machumu anasema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ulimkuta akiwa Mhariri Mtendaji wa The Citizen na ndiyo wakati alipobaini ugumu wa kusimamia gazeti nyakati hizo.
“Watu wanatafuta kushinda kwa hiyo muhimu ni namna gani mnasimama katikati, namna gani mnasimamia mwongozo wa uchaguzi, kwa hiyo kile mlichopanga kufanya kukifanya kwa uhakika wake, anasema.
Pamoja na mitihani hiyo, anasema mambo yalikwenda vema na hata walipolaumiwa ilikuwa ni kwa sababu pengine umeandikwa ukweli na si kumwonea mtu.
“Nakumbuka kuna habari moja wakati wa uchaguzi tulisema kila mtu atakayefanya mkutano apewe picha ya ukurasa wa kwanza. Kuna mgombea alifanya mkutano Buguruni alikuwa peke yake na watoto pale, ikapigwa picha ikawekwa mbele.
“Watu walichukulia kama kichekesho lakini mjadala hapa ndani ulikuwa, hivi huyu hapa anafanya kampeni au vipi, lakini tukawaeleza tuliahidi kuwapa nafasi wote,” anasema.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anasema alikuwa na nafasi ya Mhariri Mtendaji Mkuu anayesimamia magazeti yote ya MCL.
Huyu ndiye Bakari Machumu
Machumu alijiunga na MCL mwaka 2004 akiwa Mhariri wa Biashara wa The Citizen, baadaye aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo na akahudumu kwa miaka saba.
Baadaye aliteuliwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL mwenye mamlaka ya usimamizi wa magazeti yote, Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kujiunga na MCL, Machumu alifanya kazi katika kampuni ya Business Times Litd iliyokuwa inachapisha magazeti ya Majira, Business Times, Daily Times na Dar Leo kwa nafasi za uandishi na baadaye mhariri.
Kitakachokushangaza, Machumu hakuingia kuitumikia taaluma ya habari akiwa mwanataaluma hiyo, ana shahada ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) alikohitimu mwaka 1998.
Miaka 20 baadaye alipata shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA) kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uongozi ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI).
Pia, amehitimu shahada ya uzamili ya uongozi katika vyombo vya habari kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya.
Machumu alijiunga na MCL mwaka 2004 akiwa Mhariri wa Biashara wa gazeti la The Citizen, baadaye aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo na akahudumu kwa miaka saba. Baadaye aliteuliwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL mwenye mamlaka ya usimamizi wa magazeti yote, Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kujiunga na MCL, Machumu alifanya kazi katika Kampuni ya Business Times Ltd iliyokuwa inachapisha magazeti ya Majira, Business Times, Daily Times na Dar Leo kwa nafasi za uandishi na baadaye mhariri.
Kitakachokushangaza, Machumu hakuingia kuitumikia taaluma ya habari akiwa mwanataaluma hiyo, ana shahada ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) alikohitimu mwaka 1998.
Miaka 20 baadaye alipata shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA) kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uongozi ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI).
Pia, amehitimu shahada ya uzamili ya uongozi katika vyombo vya habari kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya.