CEO Namungo abwaga manyanga | Mwanaspoti

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Namungo FC, Omar Kaya ametangaza kujiuzulu wadhifa huo.

Kaya ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga, amethibitisha uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

“Mimi Omar Kaya siku ya leo Agosti 30, 2024 nimewasilisha kwa viongozi barua ya kujiuzulu nafasi ya Utendaji Mkuu wa Klabu ya NamungoFC.

“Hivyo napenda kuwashukuru viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wote wa Klabu ya Namungo katika kipindi chote nilichoitumikia klabu kwa ushirikiano wao kama familia.

“Niwatakie safari njema katika kutimiza malengo ya klabu Inshaallah,” amesema Kaya.

Mwananchi ilipomtafuta mtendaji huyo kwa njia ya simu kuthibitisha hilo amesema kuwa alichoandika kwenye mitandao yake ya kijamii ndio kilicho sahihi kisha akakata simu.

Kaya amejiweka kando katika kipindi ambacho Namungo FC imekabiliwa na matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hiyo imepoteza mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu wa 2024/2025 ilizocheza nyumbani dhidi ya Tabora United na Fountain Gate.

Timu hiyo ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 na Tabora United na kisha katika mechi iliyofuata ikachapwa mabao 2-0 na Fountain Gate.

Msimu uliopita, Namungo FC ilimaliza ikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kumaliza ikiwa imekusanya pointi 36.

Related Posts