Dodoma. Serikali imetenga Sh2.55 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya uwekaji alama na michoro ya usalama barabarani kwenye barabara kuu na za mikoa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema hayo leo Agosti 30, 2024 alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Khamis Juakali.
Mbunge huyo amehoji Serikali imejipanga vipi katika kuboresha alama za barabarani nchini kote.
Kasekenya amesema shughuli nyingine itakayofanyika ni uwekaji wa alama za watu wenye mahitaji maalumu katika mikoa yote 26.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Saurimoyo, Ali Juma Mohamed amehoji kama Serikali haioni haja ya kuweka miundombinu ya kisasa kudhibiti ajali zisitoke mara kwa mara katika maeneo ya vivukio, kwa kuwa bado kuna wimbi la ajali kwenye maeneo hayo.
Akijibu swali hilo, naibu waziri amesema kuna tatizo la watu kutofuata alama za barabarani ambazo zinafikia 183.
Amesema alama hizo ndizo zinazotumika katika nchi za Afrika Mashariki na za Kusini mwa Afrika (SADC).